BAJETI YA WIZARA YA NISHATI 2026/27 YAPITISHWA KWA KISHINDO.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limeidhinisha jumla ya shilingi trilioni 2.5 kwa ajili ya matumizi ya Wizara ya Nishati na taasisi zake katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa mwaka wa fedha 2026/2027.
Bajeti hiyo imepitishwa leo Aprili 23, 2026. Iliwasilishwa Bungeni Jijini Dodoma Jana Aprili 22, 2026 na Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi na kisha kujadiliwa na wabunge kabla ya kupitishwa rasmi leo.
Awali wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti hiyo, Ndejembi alisema kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 2.4 sawa na asilimia 97.5 ya bajeti yote ya wizara ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo huku shilingi bilioni 63 sawa na asilimia 2.5 ya bajeti ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida.
Kupitishwa kwa bajeti hiyo kunatarajiwa kuongeza kasi ya utekelezaji wa miradi ya nishati nchini, ikiwemo upanuzi wa miundombinu ya umeme na maendeleo ya vyanzo mbadala vya nishati.