Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

BAKWATA YAOMBA SERIKALI KUTOA...

BAKWATA YAOMBA SERIKALI KUTOA ELIMU KWA JAMII JUU YA MIRADI YA KIMKAKATI.

BAKWATA YAOMBA SERIKALI KUTOA ELIMU KWA JAMII JUU YA MIRADI YA KIMKAKATI.

Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limeiomba Serikali kutoa elimu ya kutosha kwa jamii ili kufahamu vema Miradi ya kimkakati inayotekelezwa nchini ukiwemo Mradi wa kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP).

Ombi hilo limetolewa na Kaimu Mufti wa Tanzania, Sheikh Ally Khamis Ngeruko, Julai 12,2023, ambaye aliongoza Viongozi wa Baraza hilo kutembelea ujenzi wa Mradi huo uliofikia asilimia 90 hadi sasa.

Mradi huo wa JNHPP unatarajiwa kukamilika Juni 14, 2024 ambapo utazalisha Megawati 2,115 zitakazoingizwa katika gridi ya Taifa ili kuongeza ufanisi wa upatikanaji wa umeme nchini.

Akizungumza na Waandishi wa habari baada ya kutembelea maeneo mbalimbali ya Mradi huo ikiwemo Kituo cha kupoza Umeme, Sheikh Ngeruko amesema ili kufanikisha suala hilo, Serikali iandae mpango maalumu wa kutoa elimu kwa jamii.

“Serikali iweke mpango mkakati wa kuelimisha jamii kuanzia ngazi ya shule za Msingi hadi Vyuo Vikuu ili kila mmoja afahamu miradi inayotekelezwa nchini, pia tunaipongeza Serikali kwa kutekeleza Mradi huu wa kuzalisha Umeme wa Julius Nyerere," amesema Sheikh Ngeruko.

Naibu Katibu wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiisalam Tanzania, Bi. Khanifa Mahamud Karamagi aliitaka jamii kuendelea kuandaa watoto kwa kuwapa elimu bora ili kuwawezesha kusimamia Miradi mikubwa inayoendelea na itakayotekelezwa nchini katika siku zijazo.

‘’Tumefurahishwa na namna ambavyo mradi huu wa kuzalisha umeme ulivyoajiri Vijana wengi wa Kitanzania, jambo ambalo linatufanya tuipongeze Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan," amesema Bi. Khanifa.

Kwa upande wake Waziri wa Nishati, Mhe. January Makamba amesema Wizara yake imetenga kiasi cha sh. bilioni 5 katika mwaka huu wa fedha kwa ajili ya masuala mbalimbali yanayohusu Mazingira, ambapo TANESCO itakuwa na jukumu la kuhakikisha vyanzo vya Maji na Mito vinalindwa.

Amefafanua kuwa fedha hizo zitatumika kutoa elimu kwa wakazi wa maeneo mbalimbali ili watunze Mazingira na wasichepushe Maji kwa lengo la kulifanya bwawa hili lidumu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 80 ijayo.

“Miaka ya nyuma hatukutenga fedha kwa lengo la kulinda mradi huu na kutoa elimu kwa Watanzania lakini sasa tumefanya hivyo kwa kuwa ukame unaosababishwa na shughuli za kibinadamu zitaathiri uzalishaji wa umeme kwenye bwawa letu,” amesema Makamba.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba amesema kuwa kazi nyingi katika mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme zimekamilika na kazi kubwa iliyobaki ipo kwenye vyumba ya mitambo ya kuzalisha umeme ambapo ujenzi wake umefikia asilimia 70 na kuanzia Februari, 2024 yataanza majaribio ya kuzungusha mitambo ya kuzalisha umeme na ifikapo mwezi Juni, 2024 umeme wa kwanza utaingizwa kwenye gridi ya Taifa.

Ziara hiyo imehudhuriwa na Viongozi kutoka Wizara ya Nishati akiwemo Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Watendaji mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la umeme Tanzania (TANESCO).