Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​BODI YA WAKURUGENZI MRADI WA...

​BODI YA WAKURUGENZI MRADI WA UMEME WA RUSUMO YAKAGUA MRADI

BODI YA WAKURUGENZI MRADI WA UMEME WA RUSUMO YAKAGUA MRADI

NA. RUBEN RICHARD- RUSUMO NGARA.

Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi kutoka Tanzania wanaosimamia mradi wa kuzalisha umeme wa Maji wa Rusumo wamefanya ukaguzi wa kazi ya ujenzi wa Mradi huo ambao kwa sasa umefikia asilimia 98.5 hadi sasa. Mradi huo unatekelezwa kwa ushirikiano wa nchi za Tanzania, Rwanda na Burundi.

Ziara hiyo, imefanyika tarehe 25, Februari 2023 ikiongozwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga kutoka Wizara ya Nishati ambaye pia ni Mjumbe wa Bodi hiyo.

Wajumbe hao wamekagua kazi mbalimbali zinazoendelea kufanyika ikiwemo ufungaji wa mitambo ya kuzalisha umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme na miradi ya kijamii ya Maji na Afya.

"Timu ya Wataalam walioko katika mradi huu mhakikishe kuwa mnashirikiana kikamilifu na Wakandarasi wa mradi ili kuhakikisha mradi huu sasa unakamilika ifikapo Juni 2023 na hakuna ucheleweshaji tena. Nchi hizi tatu za Tanzania, Burundi na Rwanda zinahitaji umeme huu wa Rusumo kwa ajili ya shughuli za kiuchumi na kijamii hivyo anzeni majaribio ya mitambo yaanze mwezi Machi na yakamilike Juni 2023. Wakandarasi mnapaswa kufanya kazi usiku na mchana bila kwenda likizo kwani huu mradi mmeuchelewesha sana” alisema Mhandisi Innocest Luoga.

Aidha, Mhandisi Luoga, alisema kuwa kila nchi imejenga miundombinu ya usafirishaji umeme ambapo kwa Tanzania tumejenga miundombinu ya Umeme kutoka Rusumo kwenda Nyakanazi.

Pia alisema kuwa miundombinu ya kusafirishaji umeme kwa upande wa Tanzania iko tayari kupokea umeme na mradi huo baada ya kukamilika utaunganishwa katika gridi ya Taifa kupitia kituo cha Nyakanazi na kuongeza kiwango cha uzalishaji umeme nchini.

Kwa Upande wake, Kamishna Msaidizi, Nuru Ndile kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Idara ya Fidia na Madeni aliweka wazi kwamba hadi Sasa malipo ya utekelezaji wa mradi huo yamefanyika kwa wakati ikiwa pamoja na fidia kwa wananchi wa eneo la mradi na Wakandarasi wa Mradi hivyo alisisitiza kukamilisha mradi kwa wakati bila kuwepo kwa visingizio vya malipo.

Pia Kamishna alisema kuwa, Mradi huo ni kielelezo cha ushirikiano wa Nchi Tatu ambazo ni Tanzania, Rwanda Na Burundi zitakazokuwa zinatumia umeme ambao utazalishwa na kugawana Kiwango Sawa cha megawati za Umeme 27 kwa kila Nchi, hivyo ni jukumu la kila nchi ni kuhakikisha fedha zilizotolewa kufadhili uwekezaji wa mradi zinatumika ipasavyo.

Wajumbe hao kutoka Tanzania pia walikagua miradi ya Kijamii ikiwemo ujenzi wa Kituo cha Afya cha Rusumo na Mradi wa Maji na kuridhishwa na kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo ya Kijamii ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Machi, 2023.