Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

DKT. BITEKO AAGIZA KITUO CHA H...

DKT. BITEKO AAGIZA KITUO CHA HUDUMA KWA WATEJA TANESCO KUSUKWA UPYA

Akerwa na kusuasua kwa utendaji wa Kituo hicho

Awataka watendaji kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea

Ahoji sababu za kutelekezwa kwa maelekezo yake ya 2024

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ameagiza kufumuliwa kwa Kituo cha Huduma kwa Wateja cha Shirika la Umeme Nchini, (TANESCO) kufuatia kituo hicho kushindwa kuwahudumia Wananchi kwa viwango vinavyotarajiwa.

Ametoa agizo hilo leo tarehe 9 Januari, 2025 jijini Dar es Salaam baada ya kutembelea kituo hicho pamoja na mambo mengine kufuatilia utekelezaji wa maelekezo yake aliyoyatoa mwezi Aprili, 2024.

Dkt. Biteko ameshangazwa na hatua ya TANESCO kuweka kando maelekezo ya mwezi Aprili 2024 yaliyolitaka Shirika hilo kuondokana namatumizi ya namba za kulipia kwenye utoaji wa huduma na kuomba namba ya bure ya huduma (free toll number) kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania -TCRA ili kuwapa unafuu wananchi wanaohitaji huduma za TANESCO.

" Wewe ulishapiga simu, pesa yako ikakatwa na huduma usiipate? Wananchi wanaumia sana!" naagiza kuundwa upya kituo ili kuongeza ufanisi na tija kwa Wananchi, "kituo hiki kinategemewa na Watanzania wengi na huduma inayotolewa hapa hairidhishi kabisa," amesema Dkt. Biteko.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Rais Samia imetoa fedha nyingi kuhudumia kituo hicho lakini utendaji wake ni mbovu kuliko huduma ya kituo.

TANESCO ilielekezwa kuachana na matumizi ya namba za kulipia Kwenye utoaji wa huduma na kuomba namba ya bure ya huduma (toll number) kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania-TCRA ili kuwapa unafuu wa Wananchi wanapopiga kuhitaji huduma za TANESCO.

Dkt. Biteko ametoa wiki moja kwa uongozi wa TANESCO kufanya maboresho ya Kituo hicho na matokeo yake yawe wazi kwa Wananchi kutokana na huduma zake.

Akizungumzia utendaji wa Kituo hicho, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mha. Abubakar Issa amesema kulikuwa na changamoto za kibajeti. Aidha amesema kwa kushirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA watakaa haraka na kuanza matumizi ya namba bila malipo ili kutoa unafuu kwa wananchi na kuleta tija kwa watumiaji.