Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

DKT. BITEKO AKUTANA NA UONGOZI...

DKT. BITEKO AKUTANA NA UONGOZI WA CHAMA CHA KIKOMUNISTI CHA CHINA

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa juu wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC)ukiongozwa na Mjumbe wa Kamati na Mkurugenzi Mkuu wa Bureau I, Idara ya Oganaizesheni ya Kamati Kuu ya Chama cha CPC, Ndugu Mao Dingzhi akiwa ameambatana na Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian

Mazungumzo hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam tarehe 28 Novemba, 2023 ambapo Ndugu Mao Dingzhi pamoja na kumpongeza Dkt. Biteko kwa kuteuliwa na kuapishwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, alizungumzia kuhusu uhusiano mzuri ulipo kati ya Tanzania na China na kushukuru jinsi Serikali ya Tanzania inavyounga mkono Serikali ya China kwenye majukwaa mbalimbali ya kimataifa.

Pamoja na kuzungumzia miradi ya Nishati, Dkt. Biteko aligusia maeneo ambayo Tanzania inahitaji ushirikiano kutoka China, ambayo ni pamoja na kujengea uwezo wataalam kwenye masuala ya utawala na teknolojia.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Bureau I na Idara ya Oganaizesheni ya Kamati Kuu ya Chama CPC, Ndugu Mao Dingzhi amesema Chama cha CPC na Chama cha Mapinduzi (CCM) vimekuwa na ushirikiano wa muda mrefu tangu enzi ya Waasisi wa vyama hivyo ambao ni Hayati Mwalimu Julius Nyerere na Mao Tse Tung na kuongeza kuwa ushirikiano huo unaendelezwa na vyama hivyo hadi sasa.

Aidha, amepongeza jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezeshaTanzania kuwa nchi ya amani, uhuru wa kutoa maoni, uzalendo na kuheshimu utu wa wananchi wake na kuahidi kuendeleza ushirikiano kwenye nyanja za uchumi wa kidijitali, masuala ya kijamii, utamaduni pamoja na elimu.