DKT. BITEKO AONGOZA WANANCHI BUKOMBE KUJIANDIKISHA DAFTARI LA MPIGA KURA
Awahimiza Kujitokeza kwa Wingi Kujiandikisha
Awataka Kutumia Haki ya Kikatiba kuchagua Viongozi Wao
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe amewahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi na kujiandikisha katika vituo vya kujiandikisha wapiga kura ili waweze kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.
Dkt. Biteko amesema hayo leo Oktoba 11, 2024 mara baada ya kujiandikisha katika Daftari la Wapiga Kura katika Kituo cha Kujiandikisha Mpiga Kura cha Shule ya Msingi Bulangwa kilichopo Wilaya ya Bukombe, Mkoa wa Geita.
“ Ninawashukuru sana kwa kujitokeza kwa wingi kujiandikisha ni jambo la muda mfupi ni imaani yangu kuwa mtamaliza kwa wakati ili muweze kwenda kuendelea na shughuli zenu,” amesema Dkt. Biteko.
Amesisitiza “ Zoezi hili linaanza leo hadi Oktoba 20, 2024. Wananchi wa Bulangwa mjitokeze waandikishaji wamejiandaa vizuri na tunataka tuone orodha ya watu wote ili muda ukifika muweze kupiga kura,” amesema Dkt. Biteko.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhe. Martine Shigella amempongeza Dkt. Biteko kwa kushiriki zoezi hilo la kujiandikisha na kusema kuwa ameonesha mfano kwa wananchi wa Bukombe na kuwataka wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ili washiriki katika uchaguzi wa kidemokrasia.
“ Tuendelee kuwasihi wananchi kutoka kila kitongoji kujiandikisha katika Daftari la Mpiga Kura kwa kuwa yametengwa maeneo ya kutosha ili kuwawezesha wananchi wote wenye sifa muweze kupata fursa hiyo,” amesema Mhe. Shigella.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukombe, Bw. Lutengano Mwalyibwa amesema kuwa maandalizi ya kibajeti na miundombinu kwa ajili ya wananchi kujiandikisha yamefanyika na kuwa Jimbo la Bukombe lina vituo 348 na mategemeo ni kuandikisha wananchi 109,124.