DKT.BITEKO ASHUHUDIA UTIAJI SAINI MIKATABA MIWILI YA KIHISTORIA YA GESI ASILIA
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko leo
 ameshuhudia uwekaji saini Mkataba wa Mauziano ya Gesi Asilia
 itakayozalishwa katika eneo la Ntorya Kitalu cha Ruvuma kilichopo
 mkoani Mtwara na uwekaji saini hati ya Makubaliano kwa ajili ya
 kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya kusambaza Gesi Asilia
 kwa teknolojia ya miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa
 Kimiminika (Mini-LNG).
 
 Hafla ya utiaji saini imefanyika tarehe 10 Januari, 2024, Wilaya ya
 Magharibi A, Mkoa wa Mjini Magharibi ambapo Mkataba wa Mauziano ya
 Gesi Asilia itakayozalishwa eneo la Ntorya umesainiwa kati ya Shirika
 la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kampuni ya ARA Petroleum ya
 Oman na Ndovu Resources ya Uingereza.Hati ya Makubaliano kwa ajili ya
 kuanzisha mahusiano ya kujenga miundombinu ya Gesi Asilia imesainiwa
 kati ya TPDC na Kampuni ya KS Energy.
 
 Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Biteko amesema kuwa, Mkakati wa
 Wizara ya Nishati ni kuhakikisha kuwa inasimamia ipasavyo Sera ya
 Nishati ya mwaka 2015 na kuhakikisha kuwa kunakuwa na upatikanaji wa
 nishati safi ambayo itawafikia wateja mbalimbali kwa urahisi na bei
 nafuu.
 
 Amesema kuwa, lengo la nchi ni kuwa na nishati inayotokana na vyanzo
 mbalimbali ikiwemo Jua, Upepo, Gesi na Maji ili Gesi Asilia iliyopo
 itumike pia kwa kiasi kikubwa kwenye maeneo mengine kama viwanda na
 majumbani badala ya kutumika kwa kiasi kikubwa kwenye umeme na pia
 kupunguza matumizi ya mafuta.
 
 “Mkakati wetu ni kubadilisha suala hili la Gesi Asilia kutumika zaidi
 kwenye umeme ambayo ni takriban asilimia 80, tunataka kuwe na nishati
 mchanganyiko nchini ili gesi itumike kwenye viwanda na majumbani na
 pia tupunguze utegemezi wa mafuta.” Amesema Dkt. Biteko
 
 Ameongeza kuwa, TPDC sasa wana mkakati utakaowezesha kuwa na mgawanyo
 wa matumizi ya Gesi Asilia ambapo matumizi kwenye umeme itakuwa
 asilimia 38, majumbani na viwandani itakuwa asilimia 32 na asilimia 10
 itabaki majumbani tofauti na ilivyo sasa ambapo matumizi ya Gesi
 viwandani na majumbani ni asilimia 28 na asilimia iliyobaki kwa kiasi
 kikubwa inaenda kwenye umeme.
 
 Kuhusu hati iliyosaniwa ya miundombinu midogo ya LNG, Dkt. Biteko
 amesema kuwa, nchi ina kilometa za mraba 945,000 na kwamba pamoja na
 uwepo wa Bomba la Gesi Asilia nchini njia rahisi ya kufanya Gesi
 iwafikie watu wengi ni kuigeuza gesi kuwa kimiminika na kusafirisha
 kwa magari kwenda kwenye maeneo ambayo watu watatumia hivyo kutiwa
 saini kwa makubaliano hayo kutawezesha Gesi kuwafikiwa wananchi wengi
 zaidi.
 
 Amesema kuwa, Serikali iko tayari kushirikiana na wawekezaji hao ili
 kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika kutoka vyanzo mbalimbali huku
 akitolea mfano utekelezaji wa mradi wa megawati 50 unaotokana na Jua
 wilayani Kishapu, Mkoa wa Shinyanga na ujenzi wa miradi mingine ya
 uzalishaji, usafirishaji na usambazaji umeme.
 
 Ameeleza kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan anafuatilia kwa karibu
 utekelezaji wa miradi ya nishati nchini kwani anachotaka ni watu
 wapate umeme wa uhakika pamoja na nishati nyinginezo.
 
 Vilevile amesema kuwa, Serikali haitaki urasimu katika utekelezaji wa
 mipango inayojiwekea kwani nia ni kwenda na wakati na kufanya vitu
 vitokee kwa manufaa ya kizazi cha sasa na cha badaye.
 
 Amesema kuwa Serikali inaangalia vitu muhimu ambavyo vitaondoa watu
 kwenye umaskini kwa haraka zaidi ikiwemo uwepo wa miundombinu ya
 barabara, anga, reli, Bandari na uwepo wa nishati ya uhakika ambapo
 kwa upande wa Wizara ya Nishati, zinafanyika kila jitihada ili kuwe na
 nishati ya kutosha na ya uhakika.
 
 Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas Ahmed
 amesema kuwa, mradi miradi hiyo ina umuhimu mkubwa ikiwemo katika
 mikoa ambapo rasilimali hiyo inazalishwa na kwamba watahakikisha
 wanaisimamia kwa ajili ya maendeleo ya Mtwara na nchi kwa ujumla.
 
 Amemshukuru, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa utekelezaji wa miradi
 mbalimbali ya kimkakati mkoani Mtwara ikiwemo ya utafutaji na
 uzalishaji wa Gesi Asilia.
 
 Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame alisema kuwa, Mkataba
 wa mauziano ya Gesi Asilia uliosainiwa leo utawezesha kuongeza gesi
 iliyogunduliwa nchini ambapo mradi huo unategemea kuzalisha kiasi cha
 kuanzia futi za ujazo milioni 60 kwa siku hadi kufikia futi za ujazo
 milioni 140 kwa siku katika kipindi cha miaka 3.
 
 Ameongeza kuwa, kukamilika kwa mkataba huu kutawezesha shughuli
 nyingine za uendelezaji kufanyika kama vile, ujenzi wa miundombinu ya
 kukusanya gesi kutoka visimani, ujenzi wa miundombinu ya kukusanya
 gesi kutoka visimani, ujenzi wa miundombinu ya usafishaji wa awali
 ikiwemo kutoa maji na ujenzi wa bomba la kilometa 34 la kusafirisha
 gesi asilia hadi kiwanda cha kuchakata gesi kilichopo Msimbati,
 Madimba mkoani Mtwara.
 
 Ameeleza kuwa, katika kitalu cha Ruvuma Gesi iliyogunduliwa na
 kuhakikiwa ni futi za ujazo bilioni 1.6.
Kuhusu Hati ya Makubaliano kwa ajili ya utekelezaji wa ujenzi wa
 miundombinu midogo ya kubadilisha Gesi Asilia kuwa kimiminika
 (Mini-LNG), ameeleza kuwa, mradi utakuwa wa kwanza kufanyika nchini na
 utawezesha kupunguza kiu ya watanzania kutumia Gesi Asilia hata kwa
 maeneo yaliyo mbali na miundombinu ya mabomba na hivyo kuchochea
 matumizi ya nishati safi nchini.
