DKT.BITEKO ATAKA UMOJA, USHIRIKIANO NA UBUNIFU TAASISI ZA NISHATI
Asema Rais Samia anataka Ubunifu ili kusogeza huduma bora kwa wananchi
Asisitiza utendaji kazi umuangalie Mtanzania wa kawaida anayeitegemea Serikali kubadili maisha
Aagiza kila Taasisi kuwa na Vigezo vya Upimaji Utendaji Kazi
Ataka Watendaji waache alama ya kazi, si kulinda vyeo
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko
amewataka Watendaji na Watumishi katika Taasisi zilizo chini ya Wizara
ya Nishati kuwa na umoja, ushirikiano na ubunifu ili kusogeza huduma
bora kwa wananchi ikiwemo za umeme, mafuta,
na Nishati Safi ya Kupikia.
Amesema hayo tarehe 28 Oktoba, 2024 jijini Dodoma wakati wa Kikao
chake na Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake
ambacho ni cha pili kutoka uanzishwe mfumo mpya ndani ya Wizara na
Taasisi zake wa kujifanyia tathmini ili kuona namna inavyofanya kazi
ya kuhudumia wananchi.
“Ikumbukwe kuwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wote amekuwa
akisisitiza kuwepo na ubunifu kwenye Wizara na Taasisi ili kusogeza
huduma za uhakika kwa wananchi na huduma hizo bora haziwezi kutokea
kama hakuna umoja na ushirikiano ndani ya Taasisi za Serikali.”
Amesema Dkt. Biteko
Katika Kikao hicho, Dkt. Biteko amewataka watendaji wa Wizara na
Taasisi kufanya kazi kwa bidii na weledi huku wakimuangalia mtanzania
wa kawaida anayetegemea mipango ya Serikali ili kuweza kubadili maisha
yake na kukumbuka kuwa Sekta ya Nishati ni injini ya uchumi wa nchi
hivyo inapotetereka yanatokea matatizo kwenye nyanja zote za kiuchumi
na hali ya maisha ya watu.
Vilevile amewakumbusha watendaji wa Wizara na Taasisi kutochukua muda
mwingi kulinda vyeo bali kinachotakiwa ni matokeo ya kazi
zitakazoacha alama kwenye Taasisi kwani vyeo huwa havidumu.
Pamoja na kupongeza Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa kuwa na
mchango katika ukuaji wa uchumi wa nchi, ametaka kila Taasisi kuwa na
Vigezo vya Upimaji wa Utendaji Kazi vitakavyotumika kufanya tathmini
ya uelekeo wa Sekta ya Nishati nchini.
Dkt. Biteko amewasisitiza Watumishi wote kutenda zaidi kuliko kusema,
kujenga taasisi imara kuliko mtu imara na kujenga Sekta ya Nishati
imara kuliko Waziri imara ili kuweza kuwahudumia wananchi vizuri na
kwa haraka.
Aidha, ameagiza Watendaji kueleza mafanikio ya Sekta ya Nishati kwa
watanzania ili wafahamu jinsi Rais Samia anavyojitoa katika
kuiendeleza Sekta ya Nishati.
Vilevile, Dkt. Biteko ameagiza kufanyike tathmini ya Mkakati wa Taifa
wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa lengo la kufahamu mwelekeo
wa utekelezaji wa mkakati huo na kuendelea kuboresha utekelezaji wake.
Katika kikao hicho cha Menejimenti ya Wizara ya Nishati na Taasisi
zake pia ilitolewa tathmini ya utendaji kazi wa Taasisi zilizo chini
ya Wizara iliyofanyika katika kipindi cha miezi mitatu kinachoishia
mwezi Septemba 2024 ambapo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umeongoza
kwa kufanya vizuri ukifuatiwa na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja
(PBPA).
Aidha, kwa tathmini ya utendaji kazi iliyofanyika ndani ya TANESCO,
mikoa ya Kitanesco ya Singida, Kinondoni Kaskazini na Manyara imefanya
vizuri zaidi katika kutoa huduma bora kwa wananchi.
Washindi wa tathmini hiyo ya utendaji kazi wamepatiwa zawadi ikiwemo
barua za pongezi huku wale ambao hawakuvuka kiwango cha asilimia 80
wakitakiwa kuongeza juhudi.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba
alisema kikao hicho ni mahsusi kwa ajili ya kufanya tathmini ya
utendaji sekta ya Nishati kwa Wizara na Taasisi zake.
Taasisi zilizoshiriki kikao hicho ni Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja
(PBPA), Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA),
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) na Kampuni ya
Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).