DKT.HOMERA AKUTANA NA KAMPUNI YA MERIDIAM KUTOKA UFARANSA KUJADILI FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA SEKTA YA NISHATI
Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa wawakilishi wa kampuni ya Meridiam kutoka Ufaransa, kujadili fursa za uwekezaji katika sekta ya nishati nchini, hususan miradi ya nishati jadidifu na miundombinu ya umeme.
Mazungumzo hayo yamefanyika leo, Novemba 20, 2026, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Nishati zilizopo Posta, Dar es Salaam.
Katika mazungumzo hayo, wawakilishi wa Meridiam for People and Planet wameonesha nia ya kuwekeza katika miradi ya nishati jadidifu inayotumia vyanzo vya maji, upepo, jua na jotoardhi, pamoja na mifumo ya kisasa ya kuhifadhi nishati kwa kutumia betri (Battery Energy Storage Systems – BESS).
Aidha, kampuni hiyo imeeleza utayari wake wa kushiriki katika ujenzi na uendelezaji wa miundombinu ya usafirishaji wa umeme (Transmission Lines), kwa lengo la kuimarisha na kupanua gridi ya taifa.
Uwekezaji huo unatarajiwa kutekelezwa kupitia utaratibu wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), utakaowezesha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya miundombinu ya nishati nchini.