The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

DKT. MATARAGIO ATOA SALAMU ZA...

DKT. MATARAGIO ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI KWA FAMILIA YA MAREHEMU KILLAGANE

Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, ametoa salamu za rambirambi kwa familia, ndugu, jamaa na wadau wa sekta ya nishati kufuatia kifo cha aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Marehemu Yona Samwel Killagane, akieleza kuwa Taifa limepoteza mtumishi mahiri aliyetoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta ya mafuta na gesi asilia nchini.

Dkt. Mataragio amesema Marehemu alitumikia Sekta ya Nishati kwa zaidi ya miaka 30, akitoa mchango mkubwa katika utafutaji na uendelezaji wa gesi asilia, tathmini za uwekezaji na majadiliano ya mikataba ya miradi mikubwa ya mafuta na gesi asilia nchini.

Amesema Marehemu ameacha urithi muhimu TPDC na Sekta ya Nishati kwa ujumla, huku akisisitiza kuwa weledi, uzoefu na kujitolea kwake katika kulitumikia Taifa vitaendelea kukumbukwa.

Kwa niaba ya Wizara ya Nishati na taasisi zake, Dkt. Mataragio ametoa pole kwa wafiwa na kuwaombea nguvu, faraja na uvumilivu katika kipindi hiki cha majonzi, huku akimuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi.