ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YATOLEWA KWA WATUMISHI WA WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO.
Wizara ya Nishati kupitia kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia leo Disemba 11, 2025 kimetoa mafunzo kwa watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo katika Ofisi za Wizara hiyo, zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma ambapo watumishi hao wameaswa kuwa mfano katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia.
Mjiolojia Nsajigwa Mwambumbuli kutoka Wizara ya Nishati amewaeleza watumishi hao juu ya faida za nishati safi, ikiwemo kupunguza athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na matumizi ya kuni na mkaa katika kupikia huku akiwaeleza Watumishi kuwa mfano wa kutumia na kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Mafunzo haya ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, hivyo dhamira ya Serikali ni kuhakikisha Taasisi za Umma zinakuwa mfano wa kuigwa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia na kupitia ninyi watumishi mtakuwa chachu ya mwamko mpana zaidi kitaifa katika matumizi ya nishati safi ya kupikia." Amesema Mwambumbuli
Ameeleza, Matumizi ya nishati isiyo safi imekuwa na athari kiafya, kiuchumi na kielimu ambapo amesema madhara hayo ni hatari kwa ustawi wa maendeleo katika jamii.
Kwa upande mwingine amesema kuwa Serikali na wadau kwa pamoja wanalenga kutimiza lengo la taifa la kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa urahisi na inawanufaisha Watanzania wote ili kuhakikisha ifikapo 2034 asilimia 80% ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake Bw. Amanzi Kimonjo ambaye ni Afisa Habari kutoka Wizara ya Nishati ameeleza Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano unalenga kuongeza uelewa wa umma na taasisi kuhusu umuhimu wa kutumia nishati safi ya kupikia.
“Mkakati wa mawasiliano umetokana na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na lengo lake ni kutoa elimu na kuwawezesha watanzania kupata taarifa sahihi na kwa urahisi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo kutokana na maendeleo ya teknolojia habari ni rahisi kuwafikia wananchi kwa kutumia redio, televisheni, pamoja na mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na twiter (x), thread, Instagram, Tik Tok, Facebook, na Youtube.
Aidha, ameongeza kuwa njia zingine za kufikisha elimu hiyo ni pamoja na kufanya kampeni mbalimbali za wazi ili kuwafikia wananchi kwa idadi kubwa
Naye Mhandisi Mwandamizi wa Utafiti kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Catherine Mwegoha ameeleza kuwa TANESCO imeendelea kutoa elimu juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia hususani nishati ya umeme kwani ni salama na nafuu kwa watumiaji hususani kwa kutumia majiko kama “Pressure Cooker” na “Induction cooker” (Jiko Janja ) kwani majiko haya yamefanyiwa utafiti na hupika vyakula vya asili kama vile ugali maharage makande na ndizi kwa kutumia umeme kidogo ukilinganisha na majiko mengine.
Akifunga Mafunzo hayo Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesisitiza umuhimu wa watumishi wa wizara hiyo kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia na kutoa pongezi kwa wawasilishaji kuhusu mada zilizowasilishwa.
“Watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo ni vyema kuwa mabalozi wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika makazi yetu na huu uelewa basi uendane na vitendo tunaporudi nyumbani tuwe wa kwanza kutumia nishati safi ya kupikia na kutoa elimu kwa wanajamii.
Katika mafunzo hayo Watumishi walipata fursa ya kuona namna jiko janja (Induction Cooker) linavyofanya kazi kwa ufaisi na kuokoa muda bila kutumia gharama kubwa.
