Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Kamati ya Kudumu Bunge ya Nis...

​Kamati ya Kudumu Bunge ya Nishati na Madini yakagua eneo la mradi wa LNG

Kamati ya Kudumu Bunge ya Nishati na Madini yakagua eneo la mradi wa LNG

Wajumbewa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini wamekagua eneo la Likong’o mkoani Lindi ambapo kutatekelezwa mradi mkubwa wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia (LNG) ikiwa ni sehemu ya ziara ya Kamati hiyo iliyolenga kukagua kazi za uzalishaji wa Gesi Asilia pamoja na miundombinu ikiwemo ya uchakataji na usafirishaji wa Gesi Asilia.

Wakiwa katika eneo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Dkt. James Mataragio, aliwaeleza Wajumbe wa Kamati hiyo kuwa, majadiliano kati ya Serikali na Wawekezaji wa mradi huo yanatarajiwa kukamilika mwezi Disemba mwaka huu.

Alisema kuwa, baada ya kukamilika kwa majadiliano hayo, kazi za awali katika eneo hilo la Likong’o zinatarajiwa kuanza mwezi Januari mwakani.

Aliongeza kuwa, wananchi waliopisha eneo hilo la mradi tayari wameshalipwa fidia ya shilingi Bilioni 5.6.

Mradi huo wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia iliyogundulika katika Bahari Kuu Kusini mwa Tanzania, utaleta nchini uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani Bilioni 40, na unatekelezwa na Kampuni ya Shell ya Uholanzi na Equinor ya Norway pamoja na washirika wao.

Wakiwa mkoani Lindi, Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, walikaguapia miundombinu ya kusafirisha gesi katika eneo la Somangafungu.

Katika eneo hilo la Somangafungu ndipo Gesi Asilia inayochakatwa Madimba mkoani Mtwara na SongoSongo mkoani Lindi zinaingia katika bomba kubwa la inchi 36 ambalo linasafirisha Gesi Asilia hadi Kinyerezi mkoani Dar es Salaam na kutumika kwa matumizi mbalimbali ikiwemo kwenye magari, majumbani, viwandani na kuzalisha umeme.