KAMATI YA NISHATI YARIDHISHWA NA BAJETI, YASISITIZA USIMAMIZI MADHUBUTI WA MIRADI.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, amesema Kamati hiyo imeishauri Serikali kuongeza ufanisi, ubunifu na usimamizi madhubuti katika usimamizi wa miradi ya nishati, ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa tija na ufanisi zaidi.
Amesema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na makadirio ya 2026/2027, ambapo aliainisha mwenendo wa bajeti, mafanikio, changamoto na mapendekezo ya kuboresha sekta hiyo.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mhe. Mgalu amesema kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Wizara ya Nishati iliidhinishiwa Shilingi 1.96 trilioni, ambapo hadi Februari 2026 ilikuwa imepokea Shilingi 1.16 trilioni, sawa na asilimia 59.28 ya bajeti yote.
Amefafanua kuwa kati ya fedha hizo, zaidi ya Shilingi 1.15 trilioni zilienda kwenye miradi ya maendeleo, huku matumizi ya kawaida yakipokea asilimia 18.9 ya bajeti iliyopangwa.
Katika eneo la mapato, Kamati imebaini kuwa Wizara ilikusanya Shilingi 6.14 milioni dhidi ya lengo la Shilingi 4 milioni, sawa na asilimia 153.5, kutokana na marejesho ya fedha za umma.
Kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Wizara ya Nishati imeomba bajeti ya Shilingi 2.52 trilioni, ikiwa ni ongezeko la takribani asilimia 44, ambapo sehemu kubwa itaelekezwa katika miradi ya maendeleo ya kimkakati.
Kamati pia imepongeza maendeleo ya miradi ya umeme vijijini kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na mradi wa umeme wa jua wa Kishapu wenye uwezo wa megawati 150, huku ikitaka Serikali kuharakisha ujenzi wa miundombinu ya gesi asilia na kuimarisha upatikanaji wa nishati nchini.