ELIMU YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA YAWAFIKIA MADIWANI WA BARIADI, SIMIYU.
Wizara ya Nishati inaendelea kuimarisha mnyororo wa thamani wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini ambapo imeanza kuwajengea uwezo Madiwani wa halmashauri mbalimbali nchini.
Wanufaika wa awali wa mpango huu ni Madiwani wa Halmashauri ya Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu ambao baada ya elimu hii watakuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo yao.
Akizungumza wakati wa semina hiyo, Bw. Ngeleja Mgejwa amesema matumizi ya nishati safi ya kupikia yana manufaa kwa jamii ikiwa ni pamoja na kuhifadhi mazingira, kulinda afya, kupunguza gharama za maisha na kuongeza muda kwa wanafamilia kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Amesema ajenda ya nishati safi ya kupikia ni ajenda ya kitaifa inahitaji ushiriki wa wadau wote, kuanzia ngazi ya wananchi hadi viongozi, ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
Bw. Mgejwa amewasihi madiwani kutumia nafasi zao kuifikisha ajenda hiyo kwa wananchi kutokana na ukaribu wao na jamii.
Kwa upande wake, Mhandisi Benezeth Kabunduguru kutoka Wizara ya Nishati, amesema Bariadi ni miongoni mwa maeneo yanayofikiwa na Serikali katika utekelezaji wa kampeni ya utoaji wa elimu kwa viongozi wa serikali za mitaa ili kuharakisha mabadiliko ya tabia kuelekea matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema madiwani wanapaswa kutumia nafasi yao ya uongozi kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia kwa kuelimisha wananchi kuhusu faida zake na kuhamasisha matumizi ya teknolojia mbalimbali za nishati safi zinazopatikana nchini.
Naye Mkurugenzi wa Mji wa Bariadi, Bw. Idd Ndabhona, ameipongeza Wizara ya Nishati kwa kuendelea kuwajengea uwezo viongozi wa ngazi ya halmashauri, akisema hatua hiyo imeongeza uelewa wao kuhusu wajibu wa kusukuma mbele ajenda ya nishati safi ya kupikia.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bariadi, Bw. Nkenyenge Chales Nkenyenge, ameishukuru Wizara ya Nishati kwa kutoa mafunzo hayo, akisema yamewaongezea viongozi uelewa na kuwapa uwezo wa kutekeleza jukumu lao la kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia katika maeneo yao.