Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Kamati ya usimamizi JNHPP yak...

​Kamati ya usimamizi JNHPP yakagua mradi.

Kamati ya usimamizi JNHPP yakagua mradi.

Ujenzi wafikia asilimia 86.8

Kamati ya Usimamizi wa Mradi wa kufua umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) imekagua mradi huo na kutoa wito kwa watanzania kuendelea kuunga mkono utekelezaji wa mradi kwakuwa una faida kubwa kwa nchi yetu na watanzania.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti ya Kamati ya Usimamizi wa mradi huo ambaye pia ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dkt. Jim Yonaz wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi huo, Mei 14, 2023 mkoani Pwani.

Ziara hiyo imehusisha Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, Makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali zinazohusika moja kwa moja katika utekelezaji wa mradi huo, Kamishna wa umeme na Nishati Mbadala kutoka Wizara ya Nishati(CERE), Mhandisi Innocent Luoga pamoja na viongozi waandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Dkt. Yonaz amesema kuwa mara baada ya mradi huo kukamilika na kuanza kuzalisha umeme, mafanikio mengine makubwa yatapatikana katika sekta ya Uvuvi, Kilimo na Utalii na hivyo kukuza uchumi wa nchi na watanzania kwa jumla.

Aidha ameipongeza Wizara ya Nishati na TANESCO kwa kazi kubwa ya usimamizi na utekelezaji wa mradi huo kwa hatua iliyofikiwa ambayo inayotoa picha halisi kwa jamii, kuwa muda si mrefu umeme utaanza kuzalishwa.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati hiyo ambaye pia ni Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba alieleza kuwa hatua ya ujenzi wa mradi huo kwa sasa umefikia asilimia 86.8 na kazi ya ujenzi inaendelea na matarajio ni kuanza kuzalisha umeme Juni 2024.

“Maendeleo ya mradi ni mazuri sana ikilinganishwa na kipindi kile ambacho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan alipokuja kuzindua rasmi zoezi la ujazaji maji katika bwawa hilo ambao eneo tulilokuwa tumekaa wakati ule kwa sasa limekuwa na maji yenye kina cha mita 30, kwa hiyo haiwezekani kufika pale tena, hiyo ni ishara inayoonesha maendeleo makubwa”, alisema Mhandisi Mramba.

Amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha na maelekezo ambayo yamewezesha mradi huo kufikia hatua hiyo, wadau mbalimbali ikiwemo Wizara ya Fedha wanaohakikisha malipo yanafanyika kwa wakati, Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa kusafirisha mitambo ya mradi huo.

Kamati hiyo imetembelea eneo la Kingo za Bwawa husika, Tuta kuu la Bwawa, nyumba ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme na njia ya kupeleka maji ya kuzungusha mitambo ya kuzalisha umeme, pamoja na eneo la ufungaji wa mitambo.