Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Kapinga: TANESCO boresheni mfu...

Kapinga: TANESCO boresheni mfumo wa utoaji huduma kwa wateja kupunguza malalamiko

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuboresha mfumo wa utoaji huduma kwa wateja ili kupunguza malalamiko na kuwapatia wananchi hao huduma ya umeme kwa wakati.

Mhe. Kapinga ametoa maelekezo hayo wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya uzalishaji wa umeme katika Kituo cha Kuzalisha Umeme Megawati 43 kwa kutumia Gesi Asilia cha Tegeta, Jijini Dar Es Salaam tarehe 2 Octoba, 2023.

Akizungumzia kituo hicho Kapinga alisema hali ya uzalishaji ni nzuri na kwamba kituo hicho kina mitambo mitano, mmoja kati ya hiyo uko kwenye matengenezo.

Amesema mfumo bora wa utoaji huduma kwa wateja hutatua changamoto ndogondogo zinazowakabili wateja majumbani kwao kama vile kuungua ama kuharibika kwa Waya, Umeme kukatika, matatizo ya LUKU pamoja na kuharibika kwa Mashineumba.

“Haipendezi na hatutakubali mwananchi yeyote alale giza kwa sababu tu hajahudumiwa licha kuwa ametoa taarifa kutokana na changamoto inayomkabili, ama changamoto yake haijatatuliwa kwa wakati, na wakati mwingine hapati majibu sahihi juu ya changamoto yake, hivyo TANESCO imarisheni mifumo yenu ili wananchi wapate huduma kwa wakati”, Amesisitiza Mhe. Kapinga.

Vilevile ameliagiza Shirika hilo kuwaunganishia umeme wananchi wote waliopo katika maeneo ambao tayari yamefikiwa na miundombinu ya umeme na uunganishwaji huo ufanyike kwa haraka na kwa wakati ili wananchi wafurahie huduma ya upatikanaji wa Umeme.

Aidha ametaka kutumika kwa mfumo wa Ni-Konekt ili kurahisisha utoaji wa huduma pia kupunguza mianya ya utoaji wa rushwa kwakuwa huduma hiyo inatolewa kwa mfumo maalum na si ana kwa ana kati ya mtoa huduma na mteja.

Akizungumzia hali ya kukatika kwa umeme katika maeneo tofauti nchini, Kapinga amewalekeza TANESCO kuzungumza na Taasisi, Viwanda na Maeneo ya uzalishaji ili kuweka mfumo wa namna bora ya kukata na kurejesha umeme katika maeneo hayo ili huduma za uzalishaji katika maeneo hayo ziendelee kutolewa.

“Haipendezi kuona maeneo ya uzalishaji yakakatwa umeme kuanzia saa kumi na mbili asubuhi hadi saa 12 jioni, ni vyema mkakubaliana muda rafiki wa kukata umeme ili kazi za uzalishaji ziweze kuendelea”, Alisema Kapinga.

Ameendelea kuwa sisitiza TANESCO, kufanya matengenezo ya lazima kwa haraka, kwa wakati na kwa muda mfupi katika mitambo yote inayopata hitilafu ili kuendeea kuimarisha hali ya upatikanaji wa huduma ya umeme nchini.

Amesema panapotokea hitilafu, hitilafu hizo zifanyike kazi kwa haraka ili umeme uendelee kupatikana kwa kuwa wananchi wanataka umeme.