Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​KATIBU MKUU NISHATI ARIDHISHW...

​KATIBU MKUU NISHATI ARIDHISHWA NA KASI YA UTEKELEZAJI MRADI WA UMEME JUA KISHAPU

Serikali kupitia Wizara ya Nishati imeeleza kuridhishwa kwake na kasi ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa kitaifa wa kuzalisha umeme jua (150MW) katika Wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga ambao hadi sasa umefikia asilimia 80.4 ya ujenzi.

Baada ya kukagua maendeleo ya mradi huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Felchesmi Mramba, amesema Serikali inaridhishwa na hatua zilizofikiwa na mkandarasi, akibainisha kuwa mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya kitaifa na kimataifa ya upatikanaji wa nishati endelevu.

Mhandisi Mramba ameeleza kuwa mradi huo wa megawati 150 unatekelezwa kwa awamu mbili kwa gharama ya Shilingi bilioni 323.

Amesema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo itakamilika desemba 2025 kwa kuanza kuzalisha megawati 50 huku Kampuni ya Sinohydro kutoka China ikiwa ndiyo mkandarasi mkuu wa mradi

“ Mradi huu ni sehemu ya jitihada za Serikali chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye anaendelea kuhakikisha kwamba Watanzania wote wanapata huduma ya nishati safi, salama na nafuu." Amesisitiza Mhandisi Mramba

Ameongeza kuwa, kukamilika kwa mradi wa umeme jua wa Kishapu kutazidi kutengemaza upatikanaji wa umeme mijini na vijijini na kupunguza utegemezi wa vyanzo vya nishati visivyo rafiki kwa mazingira.

Kwa upande wake, Mhandisi Msimamizi wa Mradi, Emmanuel Anderson amesema kasi ya ujenzi ni nzuri na wanatarajia mradi utakamilika katika muda uliopangwa.

Naye Meneja wa Kampuni ya Sinohydro, Eng. Daniel Xu, amesema dhamira ya kampuni yake ni kukamilisha mradi kwa viwango vya juu ndani ya muda uliowekwa.

“Tumeongeza nguvu kazi na vifaa kuhakikisha tunamaliza kazi kwa wakati. Tunathamini ushirikiano mzuri kutoka serikalini na wananchi wa Kishapu, tunaahidi kukamilisha mradi huu kwa ubora unaostahili." Amesema Eng. Xu

Kukamilika kwa mradi wa umeme jua Kishapu kunatarajiwa kuongeza uwezo wa nchi kuzalisha umeme wa nishati jadidifu, kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa taasisi, viwanda na wananchi, pamoja na kuchochea maendeleo ya kiuchumi katika Mkoa wa Shinyanga na taifa kwa ujumla.