The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

KILOSA MGUU SAWA UHAMASISHAJI...

KILOSA MGUU SAWA UHAMASISHAJI MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa imeahidi kushirikiana bega kwa bega na Wizara ya Nishati katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi ili kulinda mazingira na kuboresha afya za jamii.

Afisa Mazingira wa Wilaya ya Kilosa, Alex Basubizahe ametoa kauli hiyo katika mnada wa mifugo uliopo Kijiji cha Kivungu, Kata ya Kilangali wilayani Kilosa, alipokuwa akimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa wakati wa kampeni ya uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia inayoendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema matumizi ya kuni na mkaa yamekuwa yakichangia kwa kiasi kikubwa uharibifu wa mazingira, hususan ukataji miti ovyo, pamoja na kusababisha athari za kiafya kutokana na moshi unaotokana na nishati hizo.

“Ni muhimu kwa wananchi kubadili mtazamo na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia ili kuokoa misitu yetu na kulinda afya za familia zetu,” amesema Basubizahe.

Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) inaendelea na kampeni ya uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo mbalimbali nchini.

kampeni hiyo inalenga kubadilisha mtazamo wa wananchi kitabia ili wahame kutoka matumizi ya nishati isiyosafi kama kuni na mkaa na kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ikiwemo gesi, mkaa mbadala na umeme.

Katika kampeni hiyo, timu ya uhamasishaji imekuwa ikiendelea kutoa elimu pamoja na kufanya maonesho ya vitendo kwa wananchi, ikionesha namna majiko ya gesi na umeme yanavyoweza kupika kwa haraka, kwa gharama nafuu na kwa usalama zaidi.

Hatua hiyo inalenga kuongeza uelewa na mwitikio wa wananchi ili kuhamia kwa wingi katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, hatua itakayosaidia kulinda mazingira na kuboresha afya za jamii kwa ujumla.