MABADILIKO YA TABIA YA NCHI YACHOCHEA HAMASA YA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA MEATU.
Mabadiliko ya tabia ya nchi yanayoendelea kushuhudiwa nchini yameelezwa kuwa ni kichocheo muhimu cha kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, huku viongozi wakisisitiza kuwa ni wakati wa wananchi kuachana na utegemezi wa kuni na mkaa ili kulinda mazingira, afya na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa nishati.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Mhe. Antony Philipo, wakati akifungua semina ya matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Waheshimiwa Madiwani iliyoandaliwa na Wizara ya Nishati kwa lengo la kuwajengea uwezo viongozi hao kuwa mabalozi wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi katika jamii.
Mhe. Philipo amesema semina hiyo imewapa viongozi uelewa wa kina kuhusu mikakati ya Serikali ya kuhamasisha wananchi kuhama kutoka matumizi ya kuni na mkaa, ambayo siyo tu yanachangia uharibifu wa mazingira bali pia husababisha madhara mbalimbali ya kiafya kutokana na moshi unaozalishwa wakati wa kupikia.
“Lengo la semina hizi ni kutupa mikakati ya Serikali ya kuhamasisha wananchi kuhama kutoka katika matumizi ya kuni na mkaa. Sisi ni viongozi, tumekubaliana kwa pamoja kuwa tukirudi katika maeneo yetu tutahamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia,” amesema Mhe. Philipo.
Amesema kuwapa viongozi elimu ni hatua muhimu katika kuhakikisha ujumbe wa matumizi ya nishati safi ya kupikia unawafikia wananchi kwa ufanisi, akiahidi kuendelea kuisimamia ajenda hiyo ili jamii nyingi zaidi zipate uelewa na kunufaika na teknolojia za nishati safi.
Aidha, amesema ingawa mabadiliko ya tabia za matumizi yanaweza kuchukua muda, hali halisi ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi imeifanya jamii kutambua umuhimu wa kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.
“Najua haitakuwa rahisi kwa wananchi kuhama kwa sababu ni jambo geni kwa wengi, lakini wananchi wenyewe ni mashahidi wa athari za mabadiliko ya tabia ya nchi. Kwa sasa upatikanaji wa kuni na mkaa umekuwa mgumu, hivyo ni lazima tuhamie katika matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesisitiza.
Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kulinda mazingira, kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, kuboresha afya za wananchi kwa kupunguza magonjwa yanayosababishwa na moshi pamoja na kuongeza ufanisi na urahisi katika shughuli za kila siku.