The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MADIWANI SINGIDA WATAKIWA KUUN...

MADIWANI SINGIDA WATAKIWA KUUNGA MKONO JITIHADA ZA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, Mhe. Elia Digha, amewataka Waheshimiwa Madiwani kuunga mkono jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia, akieleza kuwa ushiriki wao ni muhimu katika kufanikisha utekelezaji wa agenda ya Taifa ya kuongeza matumizi ya nishati hiyo kwa wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo ya Waheshimiwa Madiwani yaliyotolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati kupitia Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Mhe. Digha amewataka Waheshimiwa Madiwani kutumia nafasi zao katika maeneo yao kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa ajenda ya nishati safi ya kupikia unahitaji ushirikiano wa viongozi katika ngazi mbalimbali, huku akibainisha kuwa Waheshimiwa Madiwani wakiwa karibu na wananchi wana nafasi kubwa ya kuhamasisha mabadiliko chanya katika matumizi ya nishati.

Mhe. Digha amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa ya kutumia nishati safi ya kupikia kwa manufaa ya afya, mazingira na maendeleo ya jamii.

Aidha, amewataka Waheshimiwa Madiwani kuendelea kuhamasisha wananchi kuhusu manufaa ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuunga mkono programu za Serikali zinazolenga kuongeza matumizi ya nishati hiyo nchini.

Kwa upande wake, Mjiolojia Mkuu kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, Bw. Ngeleja Mgejwa, amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea uelewa Waheshimiwa Madiwani kuhusu sera, mikakati na hatua zinazotekelezwa na Serikali katika kukuza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Lengo la mafunzo haya ni kuwajengea uelewa Waheshimiwa Madiwani kuhusu umuhimu wa nishati safi ya kupikia ili waweze kushiriki kikamilifu katika kutoa elimu kwa wananchi na kuhamasisha matumizi ya nishati hiyo katika maeneo yao,” amesema Bw. Mgejwa.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za Wizara ya Nishati kuwafikia Waheshimiwa Madiwani ili kuongeza uelewa na ushiriki wao katika kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi ya kupikia na kuchangia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia.