MAHUSIANO BAINA YA TAASISI NA JAMII NI CHACHU YA MAENDELEO – SALOME MAKAMBA.
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mahusiano kati ya taasisi za Serikali na jamii, akieleza kuwa ushirikiano huo ni msingi muhimu katika kuharakisha maendeleo na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Mhe. Salome ameyasema hayo, Novemba 13, 2026, alipokutana na Kampuni ya GASCO amabayo ni kampuni Tanzu ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mkuu wa Wilaya ya Mtwara pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya, kwa lengo la kujadili namna ya kuimarisha mahusiano na ushirikiano kati ya taasisi hizo na jamii.
Amesema mahusiano mazuri kati ya taasisi na jamii yameendelea kujenga imani na kuimarisha taswira ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati, akitolea mfano TPDC ambayo imepongezwa na Makamu wa Rais kutokana na shughuli mbalimbali za urejeshaji kwa jamii (CSR).
Aidha, ameipongeza pia TANESCO kwa juhudi zake katika kujenga na kudumisha mahusiano na wananchi kupitia utoaji wa huduma.
Ameeleza umuhimu wa kila taasisi kuwa na vitengo imara vya mahusiano na jamii vitakavyosimamia mawasiliano, kusikiliza changamoto za wananchi na kuhakikisha ushirikiano unakuwa endelevu.
Vilevile, amesema pongezi zinazotolewa na Wabunge kwa baadhi ya taasisi za sekta ya nishati zinaonesha umuhimu wa kuendelea kudumisha mahusiano mazuri na jamii katika utekelezaji wa majukumu na utoaji wa huduma kwa wananchi.