Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MAJALIWA: TUNATAKA TUWE WAZAL...

​MAJALIWA: TUNATAKA TUWE WAZALISHAJI WAKUBWA WA NISHATI

MAJALIWA: TUNATAKA TUWE WAZALISHAJI WAKUBWA WA NISHATI

WAZIRI MKUU, Mhe. Kassim Majaliwa leo Septemba 20, 2023 amefungua Kongamano la Tano la Nishati Tanzania ambapo amesema Serikali imedhamiria kuwawezesha Wazalishaji na Wajasiriamali katika Sekta ya Nishati, kuzalisha nishati na kuifanya Tanzania kuwa mzalishaji mkubwa wa nishati ya umeme.

Mhe. Majaliwa ameyasema hayo mara baada ya kufungua kongamano hilo la siku mbili *Septemba 20 hadi 21, 2023,* ambalo linafanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam,

“Tunaendelea na utafutaji wa gesi, tunataka tuwe wazalishaji wakubwa wa nishati, tuwe na umeme wa kutosha utakaopatikana kwa urahisi na nafuu na ziada, lakini pia Taasisi za kifedha ziko hapa zimekuja kuwahakikishia Wajasiriamali wetu kuwa wakitaka kuingia kwenye Sekta ya Nishati, mitaji ipo. Tunataka kuwa wazalishaji wakubwa wa umeme na kuuza nje ya nchi”, Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa alisema kuwa, Kongamano hilo litatoa fursa ya kupata mwelekeo wa namna ya kukabiliana na changamoto kwenye Sekta ya Nishati na namna ya kuzitatua ili kuweza kuwanufaisha Watanzania wajasiriamali na watumiaji wa nishati hiyo muhimu kwenye uchumi.

Aidha, Mhe. Majaliwa amezisisitiza nchi zote wanachama kuhakikisha taasisi za mafunzo zinatoa programu maalum za mafunzo katika Sekta za Nishati ili kuongeza idadi ya watu walio na ujuzi na maarifa kwenye Sekta hiyo.

Amesema kuwa Nishati ni Sekta muhimu katika kufikia lengo la uanzishwaji wa viwanda na katika kuimarisha na kuwezesha uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi. “Lazima tufanye kazi kwa ushirikiano na wadau wote ili kufungua fursa kwa Watanzania wote.”

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko amesema wameendelea kutekeleza mipango mbalimbali waliojiwekea katika kuhakikisha kuwa, wakati wote umeme unapatikana nchini.

Maelekezo yenu ninyi viongozi wetu juu ya kuhakikisha kuwa tuna nishati ya kutosha na ya uhakika tunaendelea nayo na tuna mipango ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu, na tuna mikakati midogo midogo ya kutuongezea umeme kipindi cha muda mrefu ambacho hakizidi miezi sita ili watu waweze kupata

umeme wa uhakika”, Alisema Dkt. Doto Biteko.

Dkt. Biteko aliwatoa hofu watanzania kuhusu nishati ya umeme kuwa, Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na wasaidizi wake wanafanya kila liwezekanalo kuhakikisha umeme unakuwepo.

Dkt. Biteko aliongeza kuwa, katika Kongamano hilo zaidi ya kampuni 100 za nishati kutoka katika maeneo mbalimbali duniani zinashiriki katika kongamano hilo ambalo lilitanguliwa na mkutano wa Viongozi wa Nishati.