The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MAJIKO BANIFU 122,776 YAMESHAS...

MAJIKO BANIFU 122,776 YAMESHASAMBAZWA NCHINI.

Wizara ya Nishati kupitia Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia imeendelea kutoa elimu kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima mkoani Simiyu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Serikali za kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Akizungumza wakati wa semina hiyo, Mhandisi Benezeth Kabunduguru, Mtaalamu kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, amesema Serikali inaendelea kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kupitia miradi mbalimbali inayolenga kuongeza upatikanaji na matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa wananchi.

Amesema hadi sasa Serikali imesambaza majiko banifu 122,776 kati ya lengo la majiko 200,000. Aidha, mitungi ya gesi ya ruzuku 359,887 kati ya lengo la mitungi 452,445 tayari imesambazwa kwa wananchi ili kuongeza upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.

Mhandisi Kabunduguru ameongeza kuwa Serikali inaendelea na utekelezaji wa hatua mbalimbali ikiwemo kuunganisha gesi asilia majumbani, kuhamasisha taasisi kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuendesha kampeni za uelimishaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Amebainisha kuwa mafanikio hayo yanaakisi dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wanapata nishati safi ya kupikia kwa gharama nafuu, hatua itakayochangia kulinda afya za wananchi, kuhifadhi mazingira na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Kwa upande wao, Waheshimiwa madiwani wameeleza kuwa semina hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu nafasi yao katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika maeneo wanayoyaongoza. Wameahidi kuendelea kutoa elimu kwa wananchi katika kata zao ili kuongeza kasi ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.