The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

“MAKAA YA MAWE RUVUMA KUZALISH...

“MAKAA YA MAWE RUVUMA KUZALISHA MEGAWATI 2,000 ZA UMEME” - DKT. HOMERA.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ametembelea eneo la mradi wa Kongani ya Viwanda unaotekelezwa na mwekezaji Hongwang Tanzania Holdings wilayani Songea, mkoani Ruvuma, unaohusisha uzalishaji wa megawati 2,000 za umeme pamoja na ujenzi wa viwanda vya aluminium na chuma.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo leo, Oktoba 23, 2026, Mhe. Homera amesema mradi huo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya uzalishaji umeme barani Afrika na kwamba unatarajiwa kuanza majaribio ya uzalishaji umeme Juni 2027.

Amesema megawati 2,000 zinazotarajiwa kuzalishwa mkoani Ruvuma, zikichanganywa na vyanzo vingine vya umeme nchini, zitachangia kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuwezesha Tanzania kufikia lengo la kuzalisha megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030, sambamba na malengo ya maendeleo ya taifa.

Aidha, Mhe. Homera amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, kwa juhudi za kuratibu shughuli za maendeleo mkoani humo. Ameeleza kuwa Wizara ya Nishati itaendelea kushirikiana na wawekezaji kuhakikisha mahitaji muhimu ya miradi ya nishati yanatekelezwa kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Waziri Homera amelielekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kukamilisha shughuli zote za kimkataba ifikapo Novemba 2026 ili kuhakikisha mwekezaji anapata megawati 200 za umeme anazohitaji kwa ajili ya kuendeleza shughuli za mradi kwa kasi iliyopangwa.

Amesisitiza kuwa hatua hiyo inaendana na dhamira ya Serikali ya kuhakikisha uwekezaji unaochochea maendeleo ya taifa unawezeshwa na miradi inatekelezwa kwa wakati.