Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Makamba aanza kazi rasmi Wizar...

Makamba aanza kazi rasmi Wizara ya Nishati

Zuena Msuya na Hafsa Omari, Dodoma

Waziri wa Nishati, January Makamba, ameanza kazi rasmi katika wizara hiyo kwa kuwataka watendaji wa wizara hiyo pamoja na Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo kufanya kazi kwa weledi wa uaminifu na uadilifu kwa maslahi mapana ya Taifa.

Amesema hayo wakati akizungumza na Uongozi wa Wizara hiyo pamoja Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya kushika wadhifa huo na kuwasili katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo katika Mji wa Magufuli Mtumba, Septemba 13, 2021.

Aliwaeleza watumishi hao kuwa anahitaji kuona matokeo chanja katika utendaji kazi pamoja na kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Kikao hicho pia kilihudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mhandisi Leonard Masanja, Naibu Katibu Mkuu, Kheri Mahimbali, Viongozi Waandamizi wa wizara pamoja na Wakuu wa Taasisi zilizochini ya Wizara hiyo.

Aidha, aliwataka watumishi hao kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuweza kusukuma mbele Sekta ya Nishati kwa lengo la kutoa huduma bora kwa wananchi na kukuza uchumi wa Taifa kwakuwa sekta hiyo ni muhimili muhimu katika kukuza uchumi wa nchi.

Sambamba na hilo amezitaka Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo,ambazo ni Shirika la Umeme Tanzania( TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini( REA), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji( Ewura), Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa pamoja( PBPA) Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania( TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Mafuta( PURA),kuhakikisha zinafanya kazi kwa kuzingatia maslahi ya nchi na watanzania kwa jumla.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato alitoa pongezi kwa Waziri Nishati kwa kuaminiwa na kuteuliwa kushika nafasi hiyo na Rais Mhe. Samia Suluhu Hasani na kwamba watumishi wa Wizara wamempokea kwa moyo mkunjufu.

Vilevile alimuhakikishia Waziri Makamba, kuwa watumishi wa Wizara pamoja na Tasisi zilizo chini ya wizara hiyo zitatoa ushirikiano mkubwa wa kiutendaji katika kuhakikisha sekta hiyo inasonga mbele na kunufaisha Taifa na watanzania kwa jumla.