Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Makamu wa Rais apongeza uteke...

​Makamu wa Rais apongeza utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere

Makamu wa Rais apongeza utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere

Ataka umakini

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango amekagua utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) na kupongeza hatua za ujenzi zilizofikiwa.

Ametoa pongezi hizo tarehe 12 Oktoba, 2021 wakati akitembelea maeneo mbalimbali ya mradi huo unaotekelezwa katika mkoa wa Pwani na Morogoro akiwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati na Mikoa ya Pwani na Morogoro wakiongozwa na Waziri wa Nishati, January Makamba.

Maeneo aliyotembelea ni pamoja na ujenzi waTuta kuu la Bwawa, Njia za kupeleka maji kwenye mitambo itakayofua umeme, Jengo la mitambo pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea na kusafirisha umeme.

“Mheshimiwa Waziri wa Nishati pamoja na TANESCO nawapongeza kwa kuendelea kusimamia ujenzi wa mradi huu, mnafanya kazi nzuri sana, Serikali inawapongeza na jicho la Serikali liko hapa kwani tuliwaahidi Watanzania kwamba tutaujenga mradi huu ili tupate umeme wa kutosha utakaojenga uchumi wa viwanda,” alisema Makamu wa Rais

Aliwataka viongozi hao kuendelea kuchapa kazi, kutanguliza uzalendo na kuwa makini ili kuhakikisha kwamba mradi huo unakamilika kwa viwango vinavyotakiwa.

Akiwa kwenye eneo unakoendelea ujenzi wa Tuta kuu la bwawa, Makamu wa Rais aliwaelekeza wasimamizi wa mradi huo kuhakikisha kuwa kila kitu kinatekelezwa kwa umakini mkubwa ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea endapo mradi huo utaanza kufanya kazi huku ukiwa na mapungufu.

“Ninyi kama wasimamizi wa mradi, mhakikishe kwamba kama kuna hitilafu inaonekana ifuatiliwe kwa ukamilifu, ikitokea tatizo lolote la kiufundi na hili bwawa likapasuka hapo baadaye madhara huko mbele yatakuwa makubwa, hatutaki kuingiza nchi yetu kwenye historia mbaya,” alisisitiza Makamu wa Rais

Aliongeza kuwa, taratibu zote za kitalaam zifuatiliwe na vigezo vizingatiwe kwa asilimia 100 na hata kama kuna hitilafu ndogo ifutiliwe chanzo chake kwa maslahi mapana ya nchi.

Alitaja gharama za utekelezaji wa mradi huo ni shilingi Trilioni 6.5 na kuwaasa watanzania kuendelea kulipa kodi ambayo ndiyo inayotekeleza miradi mikubwa kama huo wa bwawa la Julius Nyerere.

Kwa upande wa mazingira amaeagiza kuwa kuwe na usimamizi mkubwa wa masuala yote yatakayoathiri ujazaji maji katika bwawa hilo ili ndoto ya kuzalisha umeme katika bwawa hilo itimie.

“Siyo tujenge tu bwawa zuri lakini tukaja hapo baadae tukaliharibu, hivyo nawaombeni wakuu wa Mikoa, Wabunge na Wakuu wa Wilaya kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa kuhakikisha kwamba mazingira ya maeneo yanayohusu mradi huo yanabaki salama na safi ili bwawa litupatie kile tunachokitaka kama vile umeme, uvuvi na umwagiliaji na utalii,” alisema Makamu wa Rais.

Awali, Waziri wa Nishati, January Makamba, alimshukuru Makamu wa Rais kuwa, kwa kutembelea mradi huo kwani inaonesha kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita inatoa uzito na kuupa umuhimu mradi huo wa JNHPP.

Alisema kuwa, Wizara ya Nishati pamoja na TANESCO wanafahamu dhamana kubwa waliyokabidhiwa na nchi katika kusimamia mradi huo ambao una maana kubwa kwa Taifa na ni ishara na kielelezo cha maono makubwa ambayo viongozi wamekuwa nayo, kielelezo cha Taifa linalotaka kupiga hatua mbele na pia ni kielelezo cha kusukuma maendeleo na kuwajali wananchi

Alieleza kuwa, Wizara ya Nishati pamoja TANESCO wanachukulia dhamana hiyo kwa uzito mkubwa na heshima kubwa hivyo ahadi wanayoitoa ni kutimiza wajibu kwa uadilifu na weledi ili kutowaangusha Viongozi wa Nchi na watanzania kwa ujumla.

Viongozi wa Wizara ya Nishati walioambatana na Makamu wa Rais katika ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba na Wakuu wa Idara na Vitengo mbalimbali.

Moja

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango (kushoto) akisalimiana na viongozi mbalimbali wa Wizara ya Nishati, Mkoa wa Pwani na Morogoro mara alipofika katika eneo kunapotekelezwa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP). Katikati ni Mke wa Makamu wa Rais, Mbonimpaye Mpango.

Mbili

Waziri wa Nishati, January Makamba (katikati) akizungumza jambo na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango (kushoto) wakati alipotembelea mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP). Wa Pili kushoto ni Naibu Waziri wa Nishati, Stephen Byabato na kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martin Shigellah.

Tatu

Kazi za ujenzi zikiendelea katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2115.

Nne

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango (kulia) akizungumza na Waziri wa Nishati, January Makamba (katikati) na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato wakati alipofika katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kukagua utekelezaji wake.

Tano

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango (kushoto) akizungumza na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Kheri Mahimbali (wa Tatu kutoka kulia), Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Felchesmi Mramba (wa pili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande ( wa kwanza kulia) mara alipofika katika eneo la mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kukagua utekelezaji wake.

Sita

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Philip Isdor Mpango (wa Pili kushoto) akizungumza jambo wakati alipofanya ziara katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) ili kuona utekelezaji wake. Wa kwanza kushoto ni Mke wa Makamu wa Rais, Mbonimpaye Mpango, Wa Nne kutoka kushoto ni Waziri wa Nishati, January Makamba na Wa Tatu kutoka kushoto ni Mhandisi Mkazi wa Mradi wa Julius Nyerere, John Mageni.

Saba

Kazi za ujenzi zikiendelea katika mradi wa umeme wa Julius Nyerere utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2115.