The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MAKAMU WA RAIS ATAKA VIJANA KU...

MAKAMU WA RAIS ATAKA VIJANA KUNUFAIKA NA FURSA ZA MAFUTA NA GESI ASILIA.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, ameiagiza Wizara ya Nishati kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuandaa mpango mkakati utakaowezesha vijana, wanawake na kampuni za Kitanzania kunufaika na fursa za ajira, zabuni, mafunzo, teknolojia na uwekezaji katika sekta ya mafuta na gesi asilia nchini.

Mhe. Ndejembi ametoa maagizo hayo, Oktoba 28, 2026, wakati wa hafla ya utiaji saini leseni nne za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya Mnazi Bay North, West Songo Songo, Eyasi-Wembere na Lindi-Mtwara, iliyofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Amesisitiza kuwa ushiriki wa Watanzania katika sekta hiyo unapaswa kuimarishwa ili wawe sehemu ya moja kwa moja ya shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa rasilimali hizo.

Makamu wa Rais ameitaka Wizara ya Nishati kuimarisha usimamizi wa leseni hizo kwa kuweka mifumo madhubuti ya tathmini, ufuatiliaji na uwajibikaji, pamoja na kuhakikisha nidhamu ya matumizi ya fedha na kuongezeka kwa mapato ya Serikali kupitia kodi, mrabaha na mgao wa faida.

Pia ameitaka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kushirikiana na wawekezaji wenye uwezo wa kifedha, utaalamu na teknolojia ili kuongeza tija katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia.

“Uwekezaji huo una matarajio makubwa katika kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayolenga kukuza uchumi wa Tanzania kufikia thamani ya dola za Marekani trilioni moja. Vilevile, amesema maendeleo ya sekta ya gesi asilia yana nafasi muhimu katika kukidhi mahitaji ya nishati ya baadaye, ikiwemo uzalishaji wa umeme unaotarajiwa kufikia megawati 70,000 ifikapo mwaka 2050, pamoja na kukuza ajira, ujuzi na teknolojia nchini” Amesema.

Aidha, ameongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inalenga kuanzisha Kituo cha Umahiri kitakachosaidia kuendeleza ujuzi unaohitajika katika sekta ya mafuta na gesi asilia, hatua hiyo itasaidia kujenga rasilimali watu yenye ujuzi na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika shughuli za sekta hiyo na kuchochea uchumi jumuishi na endelevu.