MAKONDA: SHIMIWI IWE NAMBA MOJA NCHINI
Waziri wa Habari, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema dhamira yake ni kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuhakikisha mashindano ya Michezo ya Wizara, Taasisi na Mikoa (SHIMIWI) yanakuwa namba moja nchini.
Mhe. Makonda amesema hayo leo, Septemba 26, 2026, wakati wa ufunguzi rasmi wa mashindano ya SHIMIWI unaofanyika mkoani Kilimanjaro.
“Nataka kumuunga mkono Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha michezo yetu ya Wizara zetu, taasisi zetu na mikoa yetu inakuwa namba moja katika Taifa letu,” amesema Mhe. Makonda.
Amesema michezo siyo afya na uchumi pekee, bali pia ni nyenzo muhimu ya kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania.
Mhe. Makonda amewataka watumishi wa umma kutumia mashindano hayo kujenga umoja, mshikamano na urafiki, ili hatimaye waweze kuwatumikia wananchi kwa uadilifu na kujituma zaidi.
Kwa upande mwingine, Mhe. Makonda amesema kila kundi la mchezo linapaswa kupata zawadi zitakazokuwa alama ya ushindani na hamasa kwa washiriki.
Aidha, amewasisitiza watumishi wa umma kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuwa watumishi wema kwa Taifa, huku wakitumia michezo hiyo kuimarisha mahusiano, kutambua vipaji vya wenzao na kumtukuza Mungu kwa namna alivyowabariki.
Hafla hiyo imehudhuriwa pia na Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala (ADA), Bw. Wilson Nyamanga.