The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MASHINE UMBA ZA MVA 50 NA MVA...

MASHINE UMBA ZA MVA 50 NA MVA 20 SULUHISHO LA DHARURA KUBORESHA UPATIKANAJI WA UMEME LINDI NA MTWARA

Wizara ya Nishati imeanza kutekeleza mpango wa dharura kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa umeme wa uhakika katika mikoa ya Lindi na Mtwara, kufuatia changamoto za upatikanaji wa umeme zinazokabili mikoa hiyo.

Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ametoa hakikisho hilo alipotembelea Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Mauhumbika mkoani lindi mwishon mwa juma hili na kueleza kuwa Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tayari imeanza kuchukua hatua za haraka kutatua changamoto hiyo.

Ameeleza kuwa hatua hizo zinajumuisha kuleta mashine umba kubwa ya MVA 50 inayotarajiwa kufika Januari 2027, pamoja na mashine nyingine ya MVA 20 inayotarajiwa kufika Februari 2027. Amesisitiza kuwa jitihada zinafanyika kuhakikisha vifaa hivyo vinafika kabla ya muda uliopangwa kwa kuongeza usimamizi na kutafuta njia mbadala za usafirishaji ili kuharakisha mchakato.

Aidha, Dkt. Homera ameielekeza TANESCO Kanda kuandaa mpango mwingine wa dharura wa kuongeza uwezo wa upatikanaji wa umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara ili kupunguza athari kwa wananchi na wawekezaji wanaohitaji umeme wa uhakika kwa shughuli za uzalishaji.

Amebainisha kuwa maeneo mengine yanayokabiliwa na changamoto ya umeme ni pamoja na Tunduru, Masasi, Namyumbu, Ruangwa na Nachingwea. Hata hivyo, amesema kukamilika kwa mradi wa miundombinu ya njia ya umeme ya KV 220 Songea–Tunduru–Masasi kutamaliza changamoto hizo, sambamba na kuiunganisha mikoa hiyo katika Gridi ya Taifa.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Dkt. Homera amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, tayari imemlipa mkandarasi wa mradi wa njia ya umeme ya KV 220 Songea–Tunduru–Masasi zaidi ya Shilingi bilioni 56. Ameongeza kuwa tayari amezungumza na Waziri wa Fedha kuhakikisha fedha zilizobaki zinalipwa ili kumwezesha mkandarasi kuongeza kasi ya ujenzi na hivyo kuondoa kabisa changamoto ya umeme katika mikoa hiyo.

Akihitimisha, Dkt. Homera amesisitiza kuwa Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na TANESCO itaendelea kufanya kazi usiku na mchana kuhakikisha wananchi wanapata umeme wa uhakika bila kukatika. Aidha, amewakaribisha wawekezaji wanaotaka kuanzisha miradi katika mikoa hiyo kuanza maandalizi ya awali.

“Tutahakikisha umeme unakuwa wa uhakika na wawekezaji wanakaribishwa. Sisi kama Wizara ya Nishati tunakwenda kuhakikisha umeme wa uhakika unapatikana hapa,” ameeleza Dkt. Homera.