The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MBUNGE BAHEMU AIBUA CHANGAMOTO...

MBUNGE BAHEMU AIBUA CHANGAMOTO YA KUKATIKA UMEME NGARA, WAZIRI NDEJEMBI ATOA MWEZI MMOJA KUFUNGWA TRANSFOMA MPYA.

Mbunge wa Jimbo la Ngara, Mhe. Dotto Bahemu amesema Serikali imefanikiwa kufikisha huduma ya umeme katika vijiji vyote vya Wilaya ya Ngara, hatua inayochochea maendeleo ya wananchi na kukuza shughuli za kiuchumi wilayani humo licha ya changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara.

Mhe. Bahemu amesema pamoja na mafanikio hayo, wananchi wa Ngara bado wanakabiliwa na tatizo la kukatika kwa umeme ambalo linaendelea kusababisha usumbufu katika shughuli za kijamii na kiuchumi.

Mbunge huyo ameyasema hayo Mei 9, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Benaco hadi Kyaka pamoja na kituo cha kupoza umeme cha Benaco wilayani Ngara mkoani Kagera.

Akieleza changamoto hiyo mbele ya Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, Mhe. Bahemu amesema wananchi wa Ngara wana matumaini makubwa na mradi huo kwani utasaidia kuondoa changamoto ya kukatika kwa umeme ambayo imekuwa ikiathiri maendeleo yao kwa muda mrefu.

Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amekiri kuwepo kwa changamoto ya kukatika kwa umeme wilayani Ngara na kumuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja kunapatikana transfoma mpya yenye uwezo mkubwa ili kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika.

Aidha, Waziri Ndejembi amesema TANESCO itaendelea kufanya maboresho katika njia za kusafirisha umeme ili wananchi wa Ngara waweze kupata huduma ya uhakika wakati wakisubiri kukamilika kwa mradi huo mkubwa wa kuunganisha Mkoa wa Kagera kwenye Gridi ya Taifa.

“Wananchi wa Ngara wanataka kupata umeme wa uhakika ambao haukatikikatiki, sasa nikuagize Mkurugenzi wa TANESCO na timu yako kuhakikisha tunapata transfoma mpya mara moja yenye uwezo mkubwa ya kuhakikisha tunapata umeme katika Wilaya ya Ngara, nakupatia mwezi mmoja”. Amesema Ndejembi.

Mhe. Bahemu amefafanua kuwa pamoja na vijiji vyote 75 vya Wilaya ya Ngara kufikishiwa huduma ya umeme, vitongoji vyenye umeme ni 219 huku vitongoji 170 vikiwa bado havijafikiwa. Amesema kati ya hivyo, vitongoji 54 vipo kwenye mpango wa sasa wa kufikishiwa umeme na vitongoji 116 vinatarajiwa kufikiwa kabla ya mwaka 2030.

Katika hatua nyingine, Mhe. Bahemu ameiomba Serikali kuendelea kuwasimamia wakandarasi ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa ili dhamira ya kuunganisha Mkoa wa Kagera kwenye Gridi ya Taifa iweze kutimia.

Sambamba na hilo, amesisitiza wananchi wanaoishi katika maeneo yanayopitiwa na mradi huo kupewa kipaumbele cha ajira, hususan kwa kazi ambazo hazihitaji ujuzi maalum, hatua ambayo itasaidia kuongeza kipato kwa wananchi pamoja na kuwafanya kushiriki moja kwa moja katika utekelezaji wa mradi huo mkubwa wa maendeleo.