Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Mfuko wa Nishati Safi ya Kupi...

​Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia (CookFund) wakabidhi ruzuku ya Shilingi bilioni 3.21 kwa wasambazaji wa gesi ya mitungi

Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia (CookFund) wakabidhi ruzuku ya Shilingi bilioni 3.21 kwa wasambazaji wa gesi ya mitungi

  • Lengo ni kuchochea upatikanaji wa nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.

Mfuko wa Nishati Safi ya Kupikia (CookFund) Tanzania umetoa ruzuku yenye thamani ya Shilingi Bilioni 3.2 kwa kampuni 16 zinazojishughulisha na utoaji wa huduma za uuzaji wa nishati safi ya kupikia nchini kwa lengo la kuzisaidia kutoa huduma hizo kwa gharama nafuu na zenye ubora unaowanufaisha wateja wa kipato cha chini nchini Tanzania.

Wanufaika hao 16 ni matokeo ya mwito wa kwanza wa maombi ya ufadhili yaliyotolewa mnamo Septemba 2022 kupitia programu hiyo inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) ukilenga katika maeneo ya teknolojia safi ya kupikia hususani gesi ya ‘mitungi’ yaani Liquified Petroleum Gas (LPG), majiko ya umeme (EPC) ,majiko ya mkaa banifu (ICS) mkaa tofali utokanao na vumbi la makaa ya mawe (briquettes) na nishati ya mafuta itokanayo na mabaki ya mimea (bioethanol)

Hafla fupi ya kukabidhi hundi za fedha kwa wanufaika hao ilifanyika mkoani Dar es Salaam ikiongozwa na Waziri wa Nishati, January Makamba sambamba na Balozi wa Umoja wa Ulaya, Manfredo Fanti, na Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Mitaji wa Umoja wa Mataifa (UNCDF) Tanzania Peter Malika ambaye mfuko wake ndio unaratibu programu ya CookFund.

Akizungumza wakati wa hafla hiyo Waziri Makamba aliwasisitiza wanufaika wa ruzuku hiyo kuhakikisha wanazitumia fedha hizo kulingana na malengo ya mpango huo ili matokeo mazuri ya mpango huo yaweze kuwafikia Watanzania wengi.

“Ni vyema mkafahamu kuwa huu si mkopo bali ni ruzuku ambayo mnaipata moja kwa moja kwa jina la nchi yetu.Hivyo ni vyema mkahakikisha Watanzania wananufaika kweli kupitia mpango huu kwa kuwafikishia bidhaa zenu za nishati kwa bei nafuu ili waweze kuondokana na matumizi ya nishati chafu ambazo si rafiki kwa mazingira,’’ alisema

Akizungumzia zaidi programu ya CookFund Waziri Makamba alisema ni moja ya suluhu la msingi kwa nchi katika kupambana na matumizi ya nishati chafu kwa sababu inawahakikishia wananchi upatikanaji wa nishati safi kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Balozi Manfred Fanti aliwataka wafanyabiashara walionufaika na ruzuku hiyo kuonyesha kwamba wanaweza kuuza bidhaa zao za nishati ya kupikia kwa bei nafuu na kwa wateja wengi wapya kupitia msaada wa kifedha walioupata kupitia mpango huo

"Umoja wa Ulaya (EU) unatarajia ruzuku hizi zitasaidia watumiaji wapya wa nishati ya kupikia hapa nchini kuweza kupata vifaa vyote vinavyohusika na mfumo mzima wa zana za kupikia kwa bei nafuu na zaidi tuendelea kuhamasisha watanzania wengi zaidi waendelee kuachana na mbinu za kupikia ambazo zinachafua na kuharibu mazingira".

"Tunatumai kushuhudia matokeo ya kuridhisha katika siku zijazo na kupungua kwa familia zinazotumia nishati ya kuni au mkaa kwa kupikia." Alisema.

Akitoa shukurani zake kwa Serikali ya Tanzania na Umoja wa Ulaya, Bw. Peter Malika alisema kwa kuzingatia athari kubwa ya matumizi ya nishati itokanayo na mimea katika suala zima la mapishi nchini, ipo haja ya msingi ya kuongeza uwekezaji katika mnyororo wa thamani kwenye nishati safi ya kupikia ili kuharakisha mabadiliko kuelekea kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Kwa kuwa hii ni awamu ya kwanza ya maombi yaliyoidhinishwa ambayo yanahusisha wanufaika 16 ambao kwa jumla watahudumia kaya 191,336 katika maeneo yao na kutoa ajira 191 katika kipindi cha miaka mitatu, tunatarajia kuzindua mwito mpya wa mapendekezo mwezi huu kwa hivyo kuendelea awamu nyingine ya ruzuku kwa kama hizi,’’ alibainisha.

CookFund ni programu ya miaka mitatu inayofadhiliwa na Umoja wa Ulaya (EU) chini ya Mpango wa mkakati jumuishi wa kutumia nishati safi ya kupikia nchini na Mfuko wa 11 wa Maendeleo ya Ulaya (EDF), unaolenga kuchangia dhamira ya Tanzania ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuongeza sehemu ya idadi ya watu na upatikanaji endelevu wa ufumbuzi wa kupikia.

UNCDF ndiyo taasisi msimamizi na mtekelezaji wa programu ya CookFund. Mpango huu unalenga kushughulikia "upungufu wa mitaji" kwa upande wa watendaji wa sekta binafsi na changamoto ya kumudu gharama kwa watumiaji wa mwisho kwenye kaya.

Programu ya CookFund inachangia vipaumbele vya kimkakati vya Mfumo wa Ushirikiano wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania kwa kusaidia upatikanaji bora wa nishati safi na teknolojia, usimamizi endelevu wa maliasili na kuongeza kasi ya kazi zenye heshima katika sekta rasmi.

Kutoka Wizara ya Nishati, Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na wataalam mbalimbali.