MFUMO WA UFUATILIAJI NA TATHMINI NI NYENZO YA UTENDAJI KAZI FANISI SERIKALINI- DKT. BITEKO
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amehitimisha Kongamano la Nne la Kitaifa la Ufuatiliaji, Tathmini na Kujifunza lililofanyika Jijini Mwanza akiweka mkazo kuwa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ni nyenzo muhimu katika kuhakikisha kuwa kila taasisi inatimiza wajibu wake kwa ufanisi na hivyo kufikisha huduma bora kwa wananchi.
Kutokana na hilo, Dkt. Biteko amewataka Wataalam wa Ufuatiliaji na Tathmini nchini kufanya kazi kwa uaminifu na uadilifu bila kuogopa kuchukiwa kwani taifa linawategemea ili kuweza kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Hakuna mtu au taasisi inayoweza kufanikisha majukumu yake bila kufanya tathmini, ninyi ndio mnaoweza kutambua changamoto mapema na kuzitafutia suluhisho kabla hazijawa kubwa, taasisi yoyote inayokosa mfumo huu inafanana na timu inayoingia uwanjani bila refa.." Amesema Dkt. Biteko
Ametoa mfano kuwa katika sekta ya umeme, kabla ya kupeleka huduma hiyo eneo lolote lazima tathmni ifanyike ili kuepuka kurudia kazi mara mbili na pia tathmini husaidia kuona matokeo ya huduma husika kwa wananchi.
Kuhusu Kongamano hilo, Dkt. Biteko ameeleza kuwa mwaka jana lilihudhuriwa na washiriki 900 huku mwaka huu likivutia washiriki 1,300.
Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini (M&E) kutoka Wizara ya Nishati, Bi. Anitha Ishengoma, amesema Wizara imejipanga kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathimini ili kuboresha upatikanaji wa nishati ya uhakika na nafuu kwa Watanzania.
Ishengoma amesema Sekta ya Nishati inahusisha taasisi kubwa sita pamoja na kampuni tanzu tano ambapo kila robo mwaka Wizara hufanya vikao vya kujadili tathmini ya utendaji kazi wa Wizara na Taasisi zake vinavyoongozwa na Waziri ili kujadili masuala mbalimbali kuhusu tathmini ya utendaji kazi ikiwemo kubainisha maeneo yenye changamoto zinazojitokeza na kuweka mikakati ya kuboresha utendaji kazi.
Kongamano la Ufuatiliaji na Tathmini limewakutanisha wadau kutoka Taasisi za Umma na Sekta Binafsi kwa lengo la kuimarisha mifumo ya ufuatiliaji na tathmini kwa maendeleo endelevu.