MHE. SALOME AVUTIWA NA MATUMIZI YA NISHATI SAFI KATIKA MAONESHO YA WIKI YA NISHATI DODOMA.
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba (Mb), leo Aprili 22, 2026 ametembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Nishati yanayoendelea katika viwanja vya Bunge Jijini Dodoma, ambapo alijionea kwa karibu maendeleo ya teknolojia na ubunifu unaolenga kuimarisha matumizi ya nishati safi nchini.
Akiwa katika maonesho hayo, Mhe. Salome alijionea teknolojia ya matumizi ya gesi katika uchomaji wa nyama, jambo lililomvutia kutokana na mchango wake katika kupunguza matumizi ya nishati zisizo safi kama mkaa na kuni.
Pia alishuhudia namna gesi inavyotumika kwa ufanisi katika kupikia na kuandaa chakula, ambapo alielezwa kuwa matumizi hayo yanasaidia katika uhifadhi wa mazingira na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa unaochangia mabadiliko ya tabianchi.
Mhe. Salome aliwapongeza wadau wa sekta ya nishati kwa kuendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi, akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili wananchi wengi zaidi waweze kuhamia kwenye nishati hiyo rafiki kwa mazingira.
Wiki ya Nishati inaendelea Jijini Dodoma ikiwakutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya umma na binafsi, wakionesha teknolojia na ubunifu unaolenga kuimarisha upatikanaji na matumizi bora ya nishati nchini.