The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

MITUNGI YA GESI 359,887 YASAMB...

MITUNGI YA GESI 359,887 YASAMBAZWA NCHINI KATIKA KUENDELEZA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA.

Serikali imeendelea kuimarisha utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia kupitia miradi mbalimbali inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi kwa wananchi na taasisi, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha afya, kuhifadhi mazingira na kuchochea maendeleo ya kiuchumi.

Hayo yameelezwa na Mjiolojia Mkuu, Bw. Ngeleja Mgejwa, mtaalamu kutoka Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Wizara ya Nishati, alipokuwa akitoa mafunzo kwa Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida leo, Agosti 6, 2026.

Bw. Mgejwa amesema Serikali inaendelea na usambazaji wa mitungi ya gesi ya LPG 452,445 yenye ruzuku, ambapo hadi sasa mitungi 359,887 tayari imesambazwa kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, amesema Serikali inaendelea na mpango wa kuunganisha gesi asilia katika kaya 1,000, zikiwemo kaya 470 mkoani Lindi na 530 mkoani Pwani, pamoja na taasisi mbalimbali, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa nishati safi kwa matumizi ya nyumbani na kwenye huduma za kijamii.

Akizungumza kuhusu taasisi za umma, Bw. Mgejwa amesema Serikali imeendelea kuhamasisha taasisi kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, ambapo hadi sasa taasisi 1,472 zimehamia katika matumizi hayo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa lengo la kufikia zaidi ya taasisi 30,000 nchini.

Akihitimisha mafunzo hayo, Bw. Mgejwa amewataka Waheshimiwa Madiwani kutumia nafasi zao za uongozi kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu fursa na manufaa ya matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanatumia nishati safi, salama na yenye tija kwa maendeleo ya Taifa.