MIUNDOMBINU YA KUSAFIRISHA NA KUSAMBAZA UMEME IMEIMARIKA NCHINI
MIUNDOMBINU YA KUSAFIRISHA NA KUSAMBAZA UMEME IMEIMARIKA NCHINI
Waziri wa Nishati, January Makamba amesema kuwa hali ya miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme nchini imeimarika na hivyo kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wateja wanaotumia huduma hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Agosti 15, 2023 akiwa Dodoma wakati wa kujadili taarifa ya Wizara yake kuhusu hali ya upatikanaji wa umeme nchini kwa kipindi cha mwezi Machi hadi Agosti, 2023 kwa wajumbe wa kamati ya kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
"Miundombinu hiyo inajumuisha njia za kusafirisha umeme zenye jumla ya urefu wa kilomita 6,837 na njia ya kusambaza umeme yenye urefu wa kilomita 173,425" amesema Makamba.
Miundombinu ya kusafirisha Umeme inajumuisha kilomita 1,085 za msongo wa kV 400, kilomita 3,347 za kV 220, kilomita 1,825 za kV 132 na kilomita 580 za kV 66.
Vilevile miundombinu ya kusambaza umeme inajumuisha kilomita 56,485 za msongo wa kV 33, kilomita 12,221 za msongo wa kV 11 na kilomita 101,020 za msongo wa kV 0.4
Makamba amesema Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeunganisha wateja wapya 155, 558 ndani ya kipindi hicho ambapo uunganishaji huo umetokana na kuanzishwa kwa mfumo mpya wa maombi ya umeme wa NIkonekt na utekelezaji wa Miradi ya REA.
Waziri Makamba amesema kuwa ongezeko la wateja limewezesha wateja waliounganishiwa umeme nchini kufikia 4,443,395 ikilinganishwa na wateja 4, 287, 839 waliokuwepo kabla ya mwezi Machi, 2023 sawa na ongezeko la asilimia 3.63.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo ya Bunge Mhe. Judith Kapinga ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia TANESCO na wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa hatua zilizofikiwa katika kuimarisha miundombinu ya umeme nchini.
Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Athuman Buttuka na Watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na TANESCO.