MKAKATI WA MAWASILIANO UNATUTAKA TUWAFIKIE WANANCHI POPOTE WALIPO – MGEJWA
Mjiolojia Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Kitengo cha Nishati Safi ya Kupikia, Bw. Njeleja Mgejwa, amesema Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia unalenga kuhakikisha elimu na uhamasishaji kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia unawafikia wananchi popote walipo kupitia njia mbalimbali za mawasiliano, ikiwemo redio, runinga, magazeti na mitandao ya kijamii.
Mgejwa ameyasema hayo wakati alipotembelea kituo cha kurusha matangazo cha Standard Radio FM kilichopo Singida Mjini, ambapo alitumia fursa hiyo kutoa elimu na kuhamasisha wananchi kuhusu umuhimu wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Amesema elimu hiyo inalenga kuwahamasisha wananchi kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa lengo la kulinda afya, kuhifadhi mazingira na kuokoa muda unaotumika katika shughuli za upishi.
Aidha, Mgejwa ameeleza kuwa matumizi ya kuni na mkaa huwafanya wananchi kutumia muda na rasilimali kutafuta na kununua nishati hizo, huku matumizi yake yakichangia athari kwa afya na mazingira. Amesema ni muhimu wananchi kuelimishwa kuhusu fursa na manufaa ya kutumia nishati safi ya kupikia.