Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MKAKATI WA TAIFA WA MATUMIZI...

​MKAKATI WA TAIFA WA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA KUIMARISHA AFYA, MAZINGIRA NA UCHUMI WA NCHI

Wakati wa ufunguzi wa Mjadala wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia uliofanyika mwezi Novemba, 2022 , Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alielekeza uandaliwe Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia utakaotoa mwelekeo wa namna ya kuhamia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Mkakati huo umelenga kupunguza magonjwa ya kupumua yanayotokana na moshi, kulinda misitu, na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji katika teknolojia na vifaa safi vya kupikia.

Hayo yamebainishwa leo Novemba 20,2025 Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi wa Nishati safi ya kupikia Wizara ya Nishati Bw. Mgejwa Ngereja wakati wa kipindi cha Supa Breakfast cha East Africa Radio.

“Serikali ya Tanzania imezindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wenye lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034 hivyo, madhumuni ya Mkakati huu ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi, salama, nafuu, endelevu na ya uhakika ya kupikia”. Amehimiza Ngereja.

Aidha Ameeleza kuwa Mkakati unalenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa, kulinda afya za wananchi, kupunguza uharibifu wa misitu, na kukuza uchumi kupitia matumizi ya gesi, umeme, biogas na majiko banifu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano Serikalini Wizara ya Nishati Bi. Neema Mbuja ameeleza kuwa Mkakati wa Mawasiliano unaenda sambamba na mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwani Serikali imeanza kampeni kubwa ya kitaifa ya elimu ya uhamasishaji na mabadiliko ya tabia kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

“Katika utekelezaji wa Mkakati wa Mawasiliano wa Nishati safi ya Kupikia tumeendelea kufanya kampeni kwa kutumia redio, TV, mitandao ya kijamii, viongozi wa jamii, na taasisi mbalimbali ili kuwafikia Watanzania kote nchini kwani kuna wale wanaofikiwa moja kwa moja na wengine wanafikiwa kwa kutumia mitandao ya kijamii hususani vijana lakini pia slogani tunaenda sambamba na Slogani isemayo ‘Nishati Safi ya Kupikia Okoa Maisha na Mazingira’ ambayo imelenga kupunguza adhari za kiafya na kimazingira kwa watanzania kwa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.”Ameeleza Bi. Mbuja.

Naye, Kaimu Mkurugenzi Biashara ya Mafuta na Gesi asilia Shirika la Petroli Tanzania (TPDC)Mhandisi Emmanuel Gilbert ameeleza kuwa TPDC inaendelea kuchangia kikamilifu kupanua matumizi ya gesi asilia kama nishati safi ya kupikia kwani hadi sasa, TPDC zaidi ya kaya 3,000 zimeunganishwa kwenye mfumo wa gesi asilia katika mikoa ya Dar es Salaam, Lindi na Mtwara huku Mikoa ya Morogoro na Dodoma ikiwekwa kwenye mpango huo.

Sambamba na hilo Gilbert ameeleza kuwa elimu imeendelea kutolewa kwa umma kuhusu usalama na faida za kupikia kwa gesi ambapo jukumu la TPDC linabaki kuwa muhimu katika kufanikisha mkakati wa taifa na kupunguza matumizi ya nishati chafu kama mkaa na kuni.