MKAKATI WA TAIFA WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA UMECHOCHEA MATUMIZI YA NISHATI NCHINI
Imeelezwa kuwa Mkakati wa Taifa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia, umejikita katika kupunguza magonjwa katika mfumo wa upumuaji yanayotokana na moshi, kulinda misitu, na kuongeza fursa za kiuchumi kupitia uwekezaji katika teknolojia na vifaa vya nishati safi vya kupikia.
Hayo yamebainishwa leo Novemba 17, 2025 Jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Nishati safi ya kupikia Wizara ya Nishati Bw. Mgejwa Ngereja wakati akizungumza katika Kipindi cha Good Morning Wasafi FM.
“Tunapotekeleza mkakati mkubwa wa matumizi ya nishati safi ya kupikia tunatekeleza pia makubaliano ya kimataifa yanayolenga kupambana na mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa. dhamira ya Serikali ni asilimia 80 ya wananchi watumie nishati safi ya kupikia ifikapo 2034." Amesema Ngereja.
Amesema utekelezaji wa mkakati huo unahusisha sekta binafsi na sekta za umma huku akizitaja aina za nishati safi ya kupikia ambazo ni Umeme, nishati ya gesi(LPG), mkaa sanifu, jiko banifu, Nishati ya kinyesi cha wanyama(Bayogesi), nishati itokanayo na uchachushaji wa mabaki ya mazao ya mimea hususani mazao ya wanyama kama vile sukari na nafaka( Bayoethano) pamoja na majiko ya nishati ya jua.
Naye, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha habari na Mawasiliano Serikalini Bi. Neema Mbuja ameeleza kuwa Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano wa Nishati Safi ya Kupikia ni nyenzo muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha wananchi wanapika kwa kutumia nishati safi, salama na rafiki kwa mazingira.
" Mkakati huu wa mawasiliano umetokana na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na lengo lake ni kutoa elimu na kuwawezesha watanzania kupata taarifa sahihi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia, elimu hii wanaipata kupitia njia mbalimbali ikiwemo redio, televisheni, mitandao ya kijamii na maonyesho ya wazi," Amesema Mbuja.
Ameongeza kuwa, elimu ya nishati safi ya kupikia inatolewa kupitia mafunzo maalum kwa viongozi wa jamii, waandishi wa habari na washawishi wa mitandaoni huku akivipongeza vyombo vya habari kwa kushirikiana na waandishi wa habari kwa kuibeba ajenda ya nishati safi ya kupikia na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi wa Utafiti kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Catherine Mwegoha ameeleza kuwa Mkakati wa Taifa wa Nishati safi ya kupikia ni dhana muhimu ya kufanikisha malengo ya Taifa ya kuhakikisha usalama, uendelevu na urahisi wa upatikanaji wa nishati safi ya kupikia.
Amesema kuwa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita kutoa elimu kwa wananchi ili kuhakikisha kila mwananchi anapata uelewa juu ya faida za matumizi ya nishati safi ya kupikia pamoja na kuhakikisha wadau mbalimbali wanashirikishwa ili kuhakikisha vifaa vinawafikia wananchi kwa haraka na unafuu zaidi hususani maeneo ya Vijijini.
“Sisi kama TANESCO tunahakikisha umeme unawafikia wateja kwa kiasi kikubwa na unapatikana kwa uhakika lakini pia kwa kushirikiana na sekta binafsi tunahakikisha wananchi wanapata vifaa bora vya kupikia na vyenye gharama nafuu ili waweze kuhamia kwenye matumizi ya nishati safi ya kupikia pia tumeanzisha mfumo wa kuwapatia wananchi vifaa vya umeme ambapo kila mwezi unalipa kwa kukatwa kwenye bili ya umeme na mpaka sasa watu 480 wamenufaika”. Amesisitiza Mhandisi Mwegoha.
