Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MRADI WA GESI ASILIA UNALENGA...

​MRADI WA GESI ASILIA UNALENGA KUZALISHA, KUCHAKATA NA KUSINDIKA GESI---Byabato

MRADI WA GESI ASILIA UNALENGA KUZALISHA, KUCHAKATA NA KUSINDIKA GESI---Byabato

Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amesema Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia kuwa kimiminika unalenga kuzalisha, kuchakata na kusindika Gesi asilia iliyogunduliwa kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi kilichopo katika Mikoa ya Lindi na Mtwara.

Kauli hiyo imetolewa Agosti 16, 2023 jijini Dodoma wakati Wizara ya Nishati ilipokuwa ikiwasilisha taarifa kuhusu hatua iliyofikiwa katika Mradi wa kuchakata na kusindika Gesi Asilia kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

"Gesi Asilia iliyogunduliwa ina jumla ya futi za ujazo trilioni 45.13 ambayo ni sawa na asilimia 78.43 ya Gesi yote iliyogunduliwa nchini mpaka sasa ambayo ni futi za ujazo trilioni 57.54" amesema Byabato.

Timu ya majadiliano imeweka kipaumbele cha kuhakikisha sehemu ya gesi hiyo inabaki nchini kwa ajili ya matumizi ya ndani na hivyo kujihakikishia usalama wa nishati katika siku zijazo.

Gharama ya awali ya Mradi huo inakisiwa kufikia kiasi cha Dola za Marekani bilioni 42 ambazo ni takribani sh. trilioni 97.29 za kitanzania.

Byabato amesema Wizara ya Nishati kupitia Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) itakuwa na haki ya kushiriki kwenye mradi kama mmoja wa wabia, na utekelezaji wa mradi wa LNG umegawanyika katika hatua kuu tatu.

Kazi ya awali imekamilika ikiwemo Serikali kuridhia utekelezaji wa Mradi kwa timu za majadiliano kutoka pande zote mbili, kulipa fidia kwa wananchi watakaoathirika na mradi ambapo jumla ya sh. bilioni 5.71 zimelipwa kwa ajili ya kupisha mradi kwa eneo lenye ukubwa wa hekta 2,071.705.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Dunstan Kitandula ameipongeza Wizara ya Nishati kupitia TPDC kwa hatua iliyofikia katika kuzalisha, kuchakata na kusindika Gesi asilia iliyogunduliwa nchini.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Bw. Athumani Mbuttuka na Watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati, TPDC na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA).

.