Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​MRADI WA KUFUA UMEME WA JNHPP...

​MRADI WA KUFUA UMEME WA JNHPP KUINUA FURSA ZA KIUCHUMI NA UWEKEZAJI

MRADI WA KUFUA UMEME WA JNHPP KUINUA FURSA ZA KIUCHUMI NA UWEKEZAJI

Viongozi wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) wamesema Mradi wa kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) una manufaa makubwa kwa Taifa, licha ya kuzalisha umeme pia utaibua fursa za kiuchumi katika sekta ya utalii, kilimo na ufugaji.

Akizungumza na waandishi wa habari mara tu walipomaliza kutembelea mradi huo akiambatana na viongozi wenzake, Muasisi wa CPCT, Askofu Sylivester Gamanywa amesema fursa hizo za kiuchumi zikitumika vizuri zitaongeza tija kwenye utalii, kilimo na ufugaji kwani wananchi wengi wamejikita kwenye sekta hizo.

Katika ziara hiyo iliyofanyika Jumatano 13, 2023, Gamanywa amewahakikishia wananchi kuwa mradi wa JNHPP ni salama kwa maendeleo ya Taifa ambapo viongozi hao wametembelea maeneo muhimu ya mradi na kuona kazi zilizokamilika na zile zinazoendelea kufanyika.

“CPCT tulikuwa tunasikia tu kuhusu mradi huu lakini tumeona kazi kubwa iliyofanyika katika utekelezaji wa mradi ulioanzishwa na Serikali ya awamu ya nne na awamu ya tano inauendeleza. Ukitembelea mradi huu utajionea mambo mengi, tunaishukuru Serikali na wizara kwa kuweka utaratibu wa viongozi wa dini kuja kuona mradi unavyotekelezwa,” amesema Gamanywa.

Makamu mwenyekiti wa CPCT ambaye pia ni Askofu mkuu wa Kanisa la PAG, Daniel Awet ameishauri Serikali kuweka utaratibu wa kufanya ukarabati wa mitambo ya mradi huo mara tu itakapoanza kuzalishaji umeme ili ilete tija zaidi.

Amesema kuwa mradi huo umetumia fedha nyingi, endapo hautakarabatiwa kama ilivyopangwa itakuwa hasara kwa Taifa na itasababisha shughuli nyingi za kiuchumi kusimama.

Ameomba Serikali kutumia wataalamu wazawa ili kuhakikisha wanautunza mradi huo ambao mojawapo ya miradi mikubwa ya kuzalisha umeme katika nchi za ukanda wa Afrika mashariki.

“CPCT tumetembelea na kujionea mradi huu, tutakwenda kuwaeleza waumini wetu kuhusu umuhimu wake. Lakini tunaomba Serikali itoe elimu ya kutoa elimu kwa jamii pale inapoanzisha miradi mikubwa kama hii ili kuwajengea uelewa wa kutosha," amesema Askofu Awet.

Amesisitiza kuwa JNHPP ni mradi mkubwa wa kitaifa wenye manufaa kwa Nchi huku akiipongeza Serikali kupitia Wizara ya Nishati kwa usimamizi bora hadi hatua iliyofikiwa ya asilimia 90 ya utekelezaji.

Waziri wa Nishati, January Makamba amesema moja ya faida za mradi huo ni ujenzi wa daraja lingine kubwa katika Mto Rufiji ambalo limekamilika, akisema kwa siku zijazo wananchi wanaotoka mikoa ya kusini kwenda Dodoma hawatalazimika kupitia Dar es Salaam, bali watakatiza katika mradi huo hadi Chalinze.

“Mradi huu una faida katika sekta ya miundombinu ikiwemo ujenzi wa barabara itakayoanzia eneo la Utete mkoani Pwani kwa ajili ya kurahisisha usafiri kwa wananchi wa mikoa ya kusini na Pwani, pia mradi wa JNHPP utakuwa na manufaa kwa sekta ya maji kwa kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa urahisi,” amesema Waziri Makamba.

Waziri Makamba amesema pamoja na JNHPP, Serikali pia inatekeleza miradi mingie ya kufua umeme ukiwamo wa Rusumo unaojumuisha mataifa ya Tanzania, Rwanda na Burundi ambao ujenzi wake upo mbioni kukamilika.

Viongozi wengine wa CPCT waliokuwepo katika ziara hiyo ni Mchungaji wa Kanisa la Adventisti Wasabato, Amon Sikazwe na Mkurugenzi Idara ya wanawake CPCT, Askofu Lora Kaguo.

Pia, ziara hiyo imehudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mha.Felchesmi Mramba, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha.Innocent Luoga pamoja na Viongozi wengine kutoka Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme (TANESCO).