Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Mradi wa kufua umeme wa Kakon...

​Mradi wa kufua umeme wa Kakono kuanza

Mradi wa kufua umeme wa Kakono kuanza

Shilingi Bilioni 750 za kuendeleza mradi zasainiwa

Mradi wa kufua umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Mto Kagera (Kakono) wenye uwezo wa MW 87.8 utaanza kutekelezwa hivi karibuni baada ya kusainiwa kwa mkopo wa Dola za Marekani Milioni 325 sawa na shilingi Bilioni 750 za Kitanzania kati ya Serikali ya Tanzania na Mashirika ya Kimataifa ya Maendeleo.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba wakati wa hafla ya utiaji saini mkopo huo iliyofanyika katika ofisi ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam, Machi 15, 2023.

Amesema kuwa, fedha hizo zimetolewa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) ambayo imetoa Dola za Marekani milioni 161.47 sawa na shilingi 374.9 Bilioni, Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) limetoa Euro Milioni 110 sawa na takriban shilingi 272.6 Bilioni na Umoja wa Ulaya (EU) umetoa Euro milioni 35 sawa na shilingi 86.7 Bilioni.

Ameongeza kuwa, katika fedha hizo Serikali itatoa Dola za Marekani Milioni 6.03 sawa na takribani shilingi Bilioni 13 za Kitanzania ili kuhakikisha mradi huo unatekelezwa ndani ya kipindi cha miaka mitano kama ilivyopangwa.

Dkt.Nchemba amesema kuwa mradi wa Kakono unaendana na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP III) na sehemu ya ajenda pana ya Serikali ya Awamu ya Sita inayolenga kujenga Uchumi wa Kiushindani na uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya Watu kwa kuboresha miundombinu yenye tija, upatikanaji wa nishati ya uhakika, kuimarisha mazingira wezeshi ya biashara na uwekezaji pamoja na mifumo ya elimu na mafunzo.

“Kufuatia hatua hii muhimu iliyofikiwa, naomba kuhamasisha maandalizi ya mkataba wa Umoja wa Ulaya uharakishwe ili kuwa na fedha zote za ufadhili tayari kwa utekelezaji wa mradi”, alisema Mwigulu. Ameongeza na kusema mkataba uliobaki kusainiwa ni mmoja tu wa Umoja wa Ulaya ambapo kwa Upande wake Serikali ya Tanzania iko tayari kufanya hivyo.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Edson Ngabo amesema lengo kuu la Mradi huo ni kuongeza uzalishaji wa nishati kwenye Gridi ya Taifa kutokana na vyanzo vya gharama nafuu na pia kuongeza uhakika wa umeme katika maeneo ya Kaskazini-Magharibi mwa Tanzania hususani mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Alifafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo utakamilika ndani ya miaka mitano (5) na utahusisha ujenzi wa mtambo wa kufua umeme wa MW 87.8, njia ya kusafirishia umeme, kuboresha Kituo cha kupoza umeme na kazi nyingine zikiwemo ujenzi wa shule ya msingi na kituo cha afya katika maeneo ambayo mradi utatekelezwa.

Vilevile ujenzi wa barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 28 na hivyo kuboresha hali ya maisha ya jamii ya kanda hiyo na pia unahusisha usambazaji wa umeme na utekelezaji wa mpango wa usimamizi wa mazingira na kijamii.

Hafla hiyo imehudhuriwa na Waziri wa Fedha wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Saada Nkuya, Washirika wa Benki ya Maendeleo ya Afrika, Shirika la Maendeleo la Ufaransa na Umoja wa Ulaya na viongozi waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zake, Wizara ya Fedha na Mipango na maofisa wengine wa Serikali