Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

MRADI WA KUZALISHA UMEME KUTUM...

MRADI WA KUZALISHA UMEME KUTUMIA JUA KATIKA KIJIJI CHA NGUNGA WILAYANI KISHAPU-SHINYANGA WAFIKIA 78.5%..KAMISHNA LUOGA ASEMA NI ‘FURSA KUBWA YA MAENDELEO NA UNAFUU WA UMEME’

Serikali imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa uzalishaji umeme unaotokana na jua katika Kijiji cha Ngunga, Kata ya Talaga, Wilayani Kishapu, Mkoani Shinyanga, baada ya kufikia asilimia 78.5 ya utekelezaji wa awamu ya kwanza.

Mradi huu utazalisha Megawati 50 kwa awamu ya kwanza ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya taifa, kuongeza usambazaji wa umeme kwa wananchi.

Akizungumza Oktoba 06, 2025, Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Innocent Luoga, amesema ziara hiyo ililenga kutembelea mradi huo ili kukagua maendeleo yake na kuona jinsi unavyoweza kupunguza gharama za umeme kwa wananchi.

"Katika Awamu ya kwanza ya mradi huu utazalisha Megawati 50 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya taifa, kwa lengo la kusambaza umeme kwa wananchi na kuleta unafuu," amesema KamishnaLuoga.

Aidha, amesisitiza kuwa mradi utaendelea kufanyika kulingana na mkataba uliopo.

"Tunataka tuwe na vyanzo mbalimbali vya kuzalisha umeme, tusitegemee vyanzo vichache. Kwa sasa tunategemea maji na gesi, lakini sasa tunaanza kutumia vyanzo mbadala kama umeme wa jua, upepo, na joto la ardhi",ameeleza Kamishna Luoga.

Amefafanua kuwa kuongezwa kwa vyanzo hivi kunachangia usalama wa nishati nchini, kwani hata pale maji au gesi itakapokosekana, wananchi wataendelea kupata huduma za umeme.

Kamishna Luoga pia ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluu Hassan kwa kuweka fedha nyingi katika sekta ya nishati, jambo lililosaidia kufanikisha mradi huo.

"Kwa Mkoa wa Shinyanga, mahitaji ya umeme ni Megawati 102, lakini zipo zaidi, na uwepo wa kituo hiki unatarajiwa kuongeza megawati zaidi",amesema.

Msimamizi wa mradi, Mhandisi Emmanuel Mbando, amesema utekelezaji ulianza Desemba 8, 2023, na wanatarajia awamu ya kwanza ya Megawati 50 kukamilika ifikapo Desemba mwaka huu ili kuanza kutoa huduma kwa wananchi.

Ameongeza kuwa mradi unatekelezwa kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ni Megawati 50, kisha utekelezaji wa Megawati 100 kufikia jumla ya 150.

Mradi mzima unatarajia kugharimu shilingi bilioni 323 kwa awamu zote mbili.