Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

MRADI WA RUMAKALI (222MW) SASA...

MRADI WA RUMAKALI (222MW) SASA UNAANZA KUTEKELEZWA - DKT. BITEKO

Asema ni maagizo ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan

Ni mradi mkubwa wa umeme baada ya JNHPP

Upembuzi yakinifu wakamilika

Ruhudji (358 MW) nayo haijasahaulika

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa, mradi wa umeme wa maji wa Rumakali utakaozalisha megawati 222 uliopo wilayani Makete mkoani Njombe sasa unaanza kutekelezwa ikiwa ni utekelezaji wa maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwa, vyanzo vyote vya umeme sasa viendelezwe.

Dkt. Biteko amesema hayo tarehe 22 Februari 2024 wilayani Makete mkoani Njombe mara baada ya kutembelea eneo lenye maporomoko ya maji ya Mto Rumakali ambapo tuta la kuzuia maji yatakayozalisha umeme litajengwa pamoja na mitambo ya kuzalisha umeme

"Upembuzi yakinifu wa mradi huu ulifanyika kwa mara ya kwanza mwaka 1998 na uhuishaji wake ukafanyika mwaka 2022 ambao ulionesha kuwa mradi unatekelezeka na una manufaa ya kiuchumi na kijamii hivyo maagizo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuanza kuutekeleza ili kuongeza vyanzo vya umeme." Amesema Dkt. Biteko

Amesema kuwa, pamoja na utekelezaji wa mradi wa umeme Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha megawati 2115 lakini maendeleo makubwa yanayoendelea kutokea katika nchi yatahitaji umeme mwingi na hivyo Serikali inapata msukumo wa kuendeleza vyanzo vingine vya umeme ikiwemo mradi huo wa Rumakali.

Ameeleza kuwa, hatua inayofuata kwenye mradi huo ni utafutaji wa mjenzi ambaye atapatikana kwa njia ya ushindani wa tenda.

Amesema kuwa, mradi huo ni mkubwa na wa kielelezo kwani utatoa umeme mwingi kuliko miradi mingine ya umeme wa maji iliyopo nchini kama vile Kidatu, Kihansi, Mtera, Hale, Nyumba ya Mungu, Pangani na Rusumo hivyo Serikali imeamua kwa dhati kuutekeleza.

Ameeleza kuwa, mradi mwingine mkubwa wa maji unaoenda kutekelezwa ni mradi wa Ruhudji utakaozalisha megawati 358 uliopo mkoani Njombe na kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kutunza mazingira ambayo ndiyo yatakayopelekea uwepo wa maji ya kutosha muda wote ili kuzalisha umeme.

Ametanabaisha kuwa, vyanzo vingine mbadala vya umeme ambavyo vitaendelezwa ni pamoja na Upepo akitolea mfano mradi wa Makambako utakaozalisha megawati 600 na mradi wa umeme Jua ambao umeanza kutekelezwa wilayani Kishapu na utazalisha megawati 150.

Amesema kuwa, nia ya Serikali ni kuondoa kadhia ya kutopata umeme wa uhakika ambayo wananchi wamekuwa wakiipata ambayo inatokana na kutegemea vyanzo vichache vya uzalishaji umeme ambavyo ni Maji na Gesi Asilia.

Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amewapongeza wananchi katika Wilaya ya Makete kwa utunzaji wa mazingira ambao umepelekea mto Rumakali kuwa na maporomoko ya maji ya kutosha kuweza kuzalisha umeme.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka amesema kuwa, moja ya vipaumbele vya Mkoa huo ni utunzaji wa mazingira hivyo wamezielekeza Mamlaka za Serikali za mitaa kuweka mkazo kwenye usimamizi wa sheria ya mazingira hususani kwenye vyanzo vya maji na kuwaelekeza wananchi shughuli gani zifanyike na zisifanyike ili kutoathiri mazingira.

Mbunge wa Makete, Mhe. Festo Sanga ameipongeza Serikali kwa kuamua kutekeleza mradi huo ambapo ameeleza kuwa, toka mchakato wa utekelezaji uanze viongozi na wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakishirikishwa.

Pia ameishukuru Serikali kwa kazi ya usambazaji umeme wilayani Makete ambapo vijiji vyote 68 vina umeme na kazi iliyobaki sasa ni kusambaza umeme vitongojini.

Awali, Mratibu wa Mradi huo, Mhandisi Toto Zedekia alieleza kuwa, mradi unafaida mbalimbali ikiwemo kuchangia kuwepo kwa umeme wa kutosha na hivyo kuchangia kukua na kuendeleza sekta ya viwanda nchini na kuongeza pato la taifa kupitia viwanda.

Ameongeza kuwa, Mradi huo utasaidia kuongeza kiwango cha umeme kwenye gridi ya taifa na kuwepo kwa ajira zisizo rasmi na ajira rasmi wakati wa ujenzi, pia kuinua hali ya maisha ya wanachi wa maeneo ya mradi kupitia biashara mbalimbali.

Amesema kuwa, mradi unahusiaha pia ujenzi wa miundombinu wezeshi kama vile barabara.