Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERE...

MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE WAFIKIA ASILIMIA 80.2

MRADI WA UMEME WA JULIUS NYERERE WAFIKIA ASILIMIA 80.2

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2,115umefikia asilimia 80.2.

Naibu Waziri Byabato ameyasema hayo tarehe 17 Januari, 2023, wakati Wizara ya Nishati ikitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

“Kwa sasa utekelezaji wa mradi unaenda kwa kasiambapo hadi kufikia tarehe 31 Desemba, 2022 umefikia asilimia 80.22, aidha mnamo tarehe 22 Desemba, 2022 zoezi la kuanza kujaza maji katika bwawa la JNHPP lilifanyika kwa kufunga mageti ya njia ya mchepusho.” Amesema Byabato

Kuhusu kazi ya ujazaji maji katika Bwawa la JNHPP amesema kuwa, hadi kufikia tarehe 16 Januari, 2023 kimo cha maji cha Bwawa kilifikia mita 112.48 kutoka usawa wa bahari kutokea kimo cha mita 74 tarehe 22 Desemba 2022.

Naibu Waziri ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa JNHPP unaenda sanjari nautekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka eneo la mradi hadi Chalinze mkoani Pwanina ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ambapo kwa ujumla miradi hiyo inaendelea kutekelezwa kwa kasi.

Kuhusu malipo kwa mkandarasi wa mradi huo amesema kuwa, tayari Serikali imeshalipa asilimia 74.7 ya malipo hayo ambapo gharama za mradi huo ni shilingi Trilioni 6.5.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Dunstan Kitandula amepongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo hatuaya kuanza kujaza maji kwenye bwawa hilo. Aidha amesisitiza mradi huo kuendelea kutekelezwa kwa kasi ili asilimia za utekelezaji zilizobaki zikamilike kwa wakati.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).