Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

Naibu waziri akerwa na kasi nd...

Naibu waziri akerwa na kasi ndogo ujenzi wa kituo cha umeme

Naibu waziri akerwa na kasi ndogo ujenzi wa kituo cha umeme.

Na Timotheo Mathayo, Morogoro.

Naibu Waziri wa Nishati, Steven Byabato ametembelea ujenzi wa kituo kipya cha kupoza umeme pamoja na laini mpya za kusambaza umeme kinachojengwa wilaya ya Ifakara mkoani Morogoro.

Ziara hiyo imefanyika leo Jumatano ambapo amekagua mradi huo unaojengwa na mkandarasi AEE POWER EPC kutoka nchini Hispania.

Mkandarasi huyo anajenga kituo cha kupoza umeme wakati ambapo njia za kusambaza umeme zinajengwa na mkandarasi Burhani kutoka nchini Kenya kwa ufadhili wa umoja wa nchi za Ulaya (EU) pamoja na fedha kutoka serikali kuu ambapo jumla ya sh. bilioni kumi na nne zitatumika.

Meneja wa Tanesco wilaya ya Kilombero, Hamza Almas amesema ujenzi wa kituo cha kupoza umeme kitakuwa na mashineumba moja yenye ukubwa wa 220/33kv, 20MVA na kitatoa line kubwa za msongo wa kilovolt 33, laini moja itatoa huduma wilaya ya Ulanga na nyingine tatu zitatumika Ifakara katika wilaya ya Kilombero.

Hata hivyo Naibu waziri hakuridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa miradi huo na ametoa maelekezo kwa mkandarasi mjenzi wa mradi huo kuwepo eneo la mradi muda wote Ili akamilishe kazi kwa wakati kwa kuwa serikali serikali inamlipa kwa wakati.

Amesema Tanesco itazame taratibu zote za mkataba ili mkandarasí huyo akishidwa kutekeleza mradi kwa wakati akatwe asilimia kumi ya gharama za ujenzi wa mradi kama ilivyoainishwa katika mkataba.

Mkuu wa wilaya ya Kilombero, Hanji Godigodi amesema mara kwa mara amekuwa akifuatilia ujenzi wa mradi huo lakini mkandarasi mara nyingi amekuwa haonekani kwenye eneo la mradi, jambo linalotia hofu kama ataweza kukamilisha ujenzi kwa wakati.

Aidha Naibu waziri amefanya ziara ya kukagua bwawa la kuzalisha umeme la Kidatu kuona wingi wa maji na kama kiasi cha maji yaliyomo yataweza kukidhi mahitaji ya umeme yanayohitajika..

Byabato ameridhishwa na kiwango cha maji yaliyomo katika bwawa hilo na wataalam kutoka Tanesco wamesema ujazo uliopo katika bwawa la Kidatu kwa sasa unatosha kuzalisha umeme.