Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​Naibu Waziri wa Nishati afany...

​Naibu Waziri wa Nishati afanya ziara ya ukaguzi wa vituo vya kuzalisha umeme Ukerewe

Naibu Waziri wa Nishati afanya ziara ya ukaguzi wa vituo vya kuzalisha umeme Ukerewe

Na Timotheo Mathayo, Ukerewe.

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amefanya ziara kukagua miradi ya umeme wa gridi ndogo (mini gridi) inayozalisha na kusambaza umeme katika kisiwa cha Ukara wilayani Ukerewe katika mkoa wa Mwanza.

Ziara hiyo imefanyika Februari 27, 2022 ambapo alikutana na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya ya Ukerewe na kupokea taarifa ya upatikanaji wa umeme katika wilaya hiyo.

Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Kanali Denisa Mwila alisema kuwa hali ya upatikanaji wa umeme wilayani humo imeimarika kutokana na matengenezo makubwa yaliyofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Alisema kuwa, matengenezo hayo yalihusisha uwekaji wa waya wa majini pamoja na kusimika nguzo za chuma ndani ya eneo la Ziwa Viktoria kutoka wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Kanali Mwila alisema kuwa, zipo baadhi ya changamoto ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa umeme Jua wa 3-phase unaotekelezwa na kampuni ya JUMEME katika maeneo ambayo hayajafikiwa na TANESCO.

"Kukosekana umeme wa uhakika katika baadhi ya maeneo inaongeza shida kwa wananchi pamoja na maeneo ya kutolea huduma za jamii kama shule na zahanati." alisema Kanali Mwila

"Kuna mazungumzo yaliyofanyika kati ya Serikali na uongozi wa kampuni ya JUMEME kuhusu suala la bei ya uniti moja kuuzwa kwa sh. 100 hadi 110, lakini bado kampuni haijakubaliana na bei hiyo kutokana na madai kwamba gharama za uendeshaji wa mitambo ya kufua umeme Jua ni ghali," amesema.

Meneja wa mradi huo uliopo kisiwa cha Ukara, Ahmad Rajabu alisema kabla Serikali kutangaza bei elekezi ya mauzo ya umeme kuuzwa kwa shilingi sh. 100, kampuni ilikuwa inauza uniti moja kwa sh. 3,500 kwa watumiaji wa majumbani.

Aidha kampuni hiyo ilikuwa inawauzia umeme wafanyabiashara kwa sh. 2,500 kwa uniti ambapo watumiaji wa viwandani waliuziwa kwa sh. 750 lakini baada ya Serikali kutoa bei elekezi, wenye viwanda wananunua uniti moja kwa sh. 375.

"Mradi wa Ukara unazalisha jumla ya kilowati 180 ambapo kituo cha Bwisa kinazalisha kilowati 60, Bukiko kilowati 60 na Chifule kilowati 60." Alisema Rajabu

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato akihutubia wananchi, alisema lengo la ziara hiyo ni kukutana na wananchi ili kusikiliza maoni yao pamoja na wataalam kutoka kampuni ya kuzalisha umeme.

"Sisi kama Serikali tunakusanya maoni haya kutoka kwenu ili twende kuyafanyia kazi na hatimaye Serikali tuje na bei shirikishi itakayokuwa rafiki kati ya mwekezaji na watumiaji." alisema Byabato.

Wakati Serikali ikiendelea kulitafutia ufumbuzi suala hilo la bei ya umeme, Naibu Waziri ameitaka kampuni ya JUMEME iendelee kuuza umeme sh.100 kwa uniti moja.

Naibu Waziri alikagua mradi wa gridi ndogo 3 za umeme jua (Solar) zinazomilikiwa na kusimamiwa na kampuni ya JUMEME yenye uwezo wa kuzalisha kilowati 180 na mradi huo unahudumia wateja zaidi ya 2,500.

Alisema kuwa, maeneo ambayo hayajafikiwa na umeme ikiwemo baadhi ya vijiji na vitongoji vya Ukerewe yatapelekewa umeme, kwani Serikali inaendelea kutafuta fedha ili kuhakikisha maeneo yote nchini yanapata umeme wa uhakika ikiwemo kukamilika kwa mradi mkubwa wa Julius Nyerere.

Katika ziara hiyo Naibu Waziri alifuatana na wataalam kutoka EWURA,TANESCO, REA na wizara ya Nishati.