Tanzania emblem
The United Republic of Tanzania

Ministry of Energy

​NAIBU WAZIRI WA NISHATI AZIND...

​NAIBU WAZIRI WA NISHATI AZINDUA MPANGO WA MIAKA MINNE WA MASUALA YA JINSIA WA TANESCO

NAIBU WAZIRI WA NISHATI AZINDUA MPANGO WA MIAKA MINNE WA MASUALA YA JINSIA WA TANESCO

Naibu Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato amezindua Mpango wa miaka minne wa masuala wa jinsia wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) ambao utawezesha masuala mbalimbali ikiwemo kuboresha mfumo wa upatikanaji na utoaji wa takwimu za jinsia katika Shirika hilo.

Uzinduzi huo umefanyika tarehe 30/3/2023 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi na wadau mbalimbali wakiwemo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Athumani Mbuttuka, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Mhe.Balozi Mwanaidi Majaar na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande.

“Tumezindua programu hii ambayo itahamasisha na kusimamia haki na usawa wa watu wote katika eneo la kazi na mwisho wa siku tunataka TANESCO iwe mfano wa mashirika mengine katika kusimamia na kutekeleza masuala ya jinsia.”amesema Byabato

Amesema kuwa, katika mpango huo masuala mbalimbali yatakayofanyika ni pamoja na kuwa na sera yaTaasisi ambayo itaelekeza mambo mengi ikiwemo utaratibu kuwajengea uwezo vijana wa kike ili waweze kuingia katika kazi za kitaalam ambapo utaratibu huo utahusisha kuwatoa vijana katika vyuo na kuwapeleka kwenye Shirika na kuwapa mafunzo na baadaye kupewa ajira.

Jitihada nyingine zitakazofanyika ni kuhakikishanafasi mbalimbali katika shirika zina wanawake na vijana wa kike sawa na wanaume sambamba na kuwapeleka shule ili waongeze uelewa na ujuzi utakaowawezesha kumudu nafasi mbalimbali shirikani.

Ili mpango huo wa jinsia ufanyike kwa ufanisi, Naibu Waziri ameiagiza TANESCO kuanzisha kitengo maalum kitakachokuwa kikishughulikia masuala ya jinsia katika Shirika hilo ikiwemo malalamiko yanayohusu jinsia.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Maharage Chande amesema kuwa, suala la usawa wa kijinsia linapewa kipaumbele na TANESCO na tayari Shirika hilo limeshaweka mikakati ya kuhakikisha wanaongeza viongozi na wafanyakazi wanawake katika Shirika na kwamba Bodi pamoja na Wizara ya Nishati inawaunga mkono katika suala hilo.

“Katika utekelezaji wa suala hili la usawa wa kijinsia TANESCO tumebahatika kwani kwenye mradi wa TAZA ambao unalenga kusafirisha umeme kutoka Tanzania hadi Zambia, moja ya matakwa yake ni utekelezaji wa suala la usawa wa kijinsia, bahati nzuri suala hilo linaenda na mpango mkakati wa TANESCO hivyo sasa tunaanzasafari ya kutekeleza suala hilo ili kupunguza mwanya wa usawa wa kijinsia katika Shirika.” Amesema Chande