The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

NDEJEMBI: KIWANDA CHA NGUZO TA...

NDEJEMBI: KIWANDA CHA NGUZO TABORA KINAJIENDESHA KWA FAIDA, SERIKALI YAPANGA KUJENGA VINGINE.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuwa Kiwanda cha Kutengeneza Nguzo za Zege cha TCPM kilichopo mkoani Tabora kinajiendesha kwa faida, hali inayokifanya kuwa chachu ya kuanzishwa kwa viwanda vingine zaidi nchini.

Mhe. Ndejembi ametoa kauli hiyo Machi 12, 2026 wakati Kamati hiyo ilipotembelea na kukagua kiwanda hicho kinachomilikiwa na Serikali kupitia kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), yaani Tanzania Concrete Poles Manufacturing Company (TCPM).

Amesema hadi sasa Serikali imeshasimika takribani nguzo za zege 120,000 katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya mpango wa kuunganisha wateja wapya 1,300,000 wa umeme kila mwaka. Kwa sasa, idadi ya wateja wa umeme nchini imefikia takribani milioni tano.

“Pamoja na kukamilika kwa kiwanda hiki, bado kuna nafasi kubwa kwa sekta binafsi kushiriki kwa kuanzisha viwanda zaidi. TANESCO huwasilisha mahitaji ya nguzo kwa TCPM, na baada ya kuangalia uwezo wake wa uzalishaji, mahitaji yaliyobaki hupewa makampuni binafsi,” amesema Mhe. Ndejembi.

Ameongeza kuwa bado kuna fursa kubwa kwa wawekezaji binafsi kuanzisha viwanda vya kutengeneza nguzo za zege, kwani mahitaji yake yanaendelea kuongezeka kutokana na jitihada za Serikali za kupanua miundombinu ya umeme nchini.

Kwa mujibu wa Waziri huyo, kiwanda hicho kimegharimu takribani shilingi bilioni 7.9 kukamilika na kina uwezo wa kuzalisha nguzo za zege kati ya 80 hadi 120 kwa siku.

Aidha, Serikali inapanga kujenga viwanda vingine kama hicho katika mikoa mbalimbali ili kuongeza uzalishaji wa nguzo za umeme, kuboresha miundombinu ya nishati na kupunguza changamoto za upatikanaji wa umeme nchini.