The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

NDEJEMBI: MoU YA TANZANIA NA U...

NDEJEMBI: MoU YA TANZANIA NA UGANDA KUIFANYA TANGA KITOVU CHA NISHATI AFRIKA MASHARIKI.

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema kusainiwa kwa Hati ya Makubaliano (MoU) kati ya Serikali za Tanzania na Uganda kuhusu Uendelezaji wa Kituo Kikuu cha Nishati cha Tanga (Tanga Regional Energy Hub) ni hatua ya kimkakati itakayobadili sura ya uchumi na sekta ya nishati katika Afrika Mashariki kwa kuvutia uwekezaji unaokadiriwa kuzidi dola za Marekani bilioni 20 na kuongeza thamani ya rasilimali za mafuta katika ukanda huo.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam leo, Alhamisi Agosti 6, 2026, katika hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo iliyoshuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Mhe. Ndejembi amesema hatua hiyo inaonesha uwezo wa nchi za Afrika kushirikiana kama washirika wa kimkakati katika kupanga, kugharamia na kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo yenye manufaa ya pamoja.

Amesema ushirikiano huo umejengwa juu ya mafanikio ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) wenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni sita, ulioanzishwa mwaka 2017 kati ya Tanzania, Uganda na washirika wao. Ameeleza kuwa Tanga imechaguliwa kuwa kitovu hicho kutokana na ubora wake wa kiufundi, kiuchumi, kimazingira na nafasi yake ya kimkakati katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Mhe. Ndejembi amesema hatua inayofuata si kusafirisha mafuta ghafi pekee, bali kujenga uchumi unaoongeza thamani ya rasilimali hizo kupitia usafishaji wa mafuta, uhifadhi, biashara, usafirishaji, maendeleo ya viwanda, ajira na biashara ya kikanda. Amebainisha kuwa hatua hiyo ni utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuifanya Tanga kuwa kitovu cha mafuta na nishati kwa Afrika Mashariki.

Amefafanua kuwa Tanga ina sifa za kipekee zinazoifanya kuwa eneo sahihi kwa mradi huo, ikiwemo kuwa lango la EACOP, kuwa na ufukwe wa Bahari ya Hindi, miundombinu bora ya bandari, maeneo ya viwanda pamoja na mtandao wa usafiri unaounganisha Afrika Mashariki, Kati na Kusini, hali inayoiweka katika nafasi nzuri ya kuwa kitovu cha biashara ya nishati katika soko linalokua kwa kasi.

Aidha, amesema mradi wa Tanga Regional Energy Hub haupingani na mpango wa Uganda wa kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta, bali miradi hiyo itakamilishana. Amesema ushirikiano huo utaimarishwa kupitia ujenzi wa bomba la kisasa la kusafirisha bidhaa za mafuta kati ya Tanga na Uganda, litakalowezesha mafuta yaliyosafishwa kusafirishwa kwa ufanisi kulingana na mahitaji ya masoko ya Tanzania, Uganda, Rwanda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Sudan Kusini na masoko ya kimataifa kupitia Bandari ya Tanga.

Amesisitiza kuwa kusainiwa kwa MoU hiyo ni mwanzo wa maandalizi ya utekelezaji wa miradi itakayovutia uwekezaji mkubwa, kuongeza ajira, kukuza ujuzi, kuharakisha uhamishaji wa teknolojia na kupanua fursa za biashara kwa wahandisi, wataalamu na vijana wa Afrika. Amesema hatua hiyo pia itawezesha Tanzania na Uganda kushiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya mafuta na kuimarisha ushindani wa ukanda wa Afrika Mashariki katika soko la kimataifa la nishati.