The United Republic of Tanzania
Ministry of Energy

NDEJEMBI: TUTATIMIZA MAONO YA...

NDEJEMBI: TUTATIMIZA MAONO YA RAIS SAMIA YA KUZALISHA MW 8,000.

Wizara ya Nishati imesisitiza kuwa ipo katika mkakati madhubuti wa kutimiza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kufikisha uzalishaji wa umeme Megawati 8,000 ifikapo mwaka 2030.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni na Waziri wa Nishati,Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akijibu hoja za wabunge na kuhitimisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara pamoja na taasisi zake kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Alieleza kuwa mwaka 2021, Rais Samia alipoingia madarakani, uzalishaji wa umeme nchini ulikuwa megawati 1,540, lakini kwa sasa umeongezeka na kufikia takribani megawati 4,500.

“Tutafikia lengo la megawati 8,000 ifikapo 2030, na hili linawezekana. Tutatumia vyanzo mbalimbali vya nishati ikiwemo maji, jua, upepo na makaa ya mawe,” alisema Ndejembi.

Katika kuongeza uzalishaji kupitia vyanzo vya maji, Wizara inaendelea kutekeleza miradi kadhaa muhimu ikiwemo Malagarasi (MW 49), Kakono (MW 87), Ruhudji (MW 358) pamoja na Rumakali (MW 222).

Aidha, Serikali imeweka mkakati wa kuendeleza nishati jadidifu, hususan jotoardhi (geothermal), ambapo inalenga kuzalisha megawati 130 ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wa makaa ya mawe, Ndejembi alisema Tanzania ina akiba kubwa, na serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inalenga kuzalisha zaidi ya Megawati 2,000 kupitia chanzo hicho.

Katika sekta ya nishati ya jua, mradi wa Kishapu mkoani Shinyanga tayari umeanza kuingiza umeme katika gridi ya taifa, ukitarajiwa kuongeza zaidi ya Megawati 100. Miradi mingine inaandaliwa katika maeneo ya Manyoni na Dodoma.

Vilevile, miradi ya nishati ya upepo inatarajiwa kutekelezwa katika maeneo ya Same na Makambako.

Serikali pia inapanga kuanza matumizi ya teknolojia ya kuhifadhi umeme (battery storage) ili kuongeza ufanisi wa nishati jadidifu.

Kwa upande mwingine, Wizara ipo katika hatua za awali za kuchunguza uwezekano wa kuzalisha umeme kwa kutumia madini ya urani, ikiwa ni jitihada za kupanua zaidi vyanzo vya nishati nchini.